Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )
Ushuhuda
Ushuhuda

Naitwa Rehema Chalamila, wengi wananifahamu kwa jina la Kisanii la “Ray C”. Mungu alinibariki na kuwa mtu mwenye mafanikio makubwa kwani nikiwa na umri wa miaka 17 nilifanikiwa kupata kazi ya utangazaji katika Radio East Africa, mwaka 1999, mwaka 2000 nilijiunga na Radio Clouds. Mafanikio yangu hayakuishia hapo, nikiwa Radio Clouds mwaka 2002 nilianza muziki na kupata mafanikio makubwa sana. Mafanikio ambayo yaliniwezesha kujenga nyumba nzuri na kubwa nikiwa na umri wa miaka 19, baadaye kununua magari na kufungua maduka makubwa jijini Dar es Salaam na hatimaye kuwa msaada mkubwa wa familia yetu.

Aidha, nilitembelea Nchi nyingi duniani kufanya muziki. Ghafla ujana ulionipaisha na kunipeleka juu ukanigeuza kichwa chini miguu juu. Uwezo wangu wa kufanya muziki ulitoweka, nilianza kuuza vitu vyangu kimoja baada ya kingine nikianza na vidogo vidogo, mwisho nikauza magari yangu, Nyumba nayo ikaenda, Maduka nayo nikayafilisi nikafunga, nikaanza kuwa mtu wa kujificha huku nikendelea kudhoofika.

Ilifika wakati nililazimika kutembea nimevaa “kininja”. Dawa za kulevya zilikuwa zinanimaliza! Nilipokuja kushtuka nilikuwa tayari nimenasa, Maisha yangu yakawa si starehe tena bali mateso na aibu! Nilipokuwa katika uteja nilikwenda mbali zaidi ya kuuza vitu vyangu vya thamani. Roho inaniuma sana ninapokumbuka nilipomshikia kisu mama yangu mzazi kumlazimisha anipe hela nikanunue dawa. Roho inaniuma sana ninapokumbuka nilipomnyonga mkono mama kumpokonya simu.. ninapokumbuka haya roho huwa inaniuma kuliko hata kupoteza vitu vyangu vya thamani nilivyopoteza.