(DCEA)
BANGI NI NINI?
Bangi ni aina ya dawa ya kulevya inayotokana na mmea unaoitwa “Cannabis sativa” ambao hustawi na hutumika kwa wingi hapa nchini na duniani kote. Bangi huathiri ubongo na kubadili jinsi tunavyotafsiri uhalisia wa vitu. Majani na maua ya mmea huo hukaushwa na hutumiwa kama kilevi peke yake au kwa kuchanganywa na dawa zingine. Mara nyingi bangi imekuwa ni kati ya dawa ya awali kutumiwa, ambapo watumiaji wengi huanza matumizi wakiwa na umri mdogo hivyo kuwa katika hatari zaidi kiafya, kijamii na kiuchumi. Aidha, watumiaji wengi wa bangi huishia kutumia dawa nyingine hapo baadae kama heroin na cocaine. Hivyo, bangi hutumika kama njia ya kuingia katika matumizi ya dawa nyingine za kulevya. Majina mengine ya bangi yanayotumika mitaani ni kama msuba, dope, nyasi, majani, mche, kitu, blanti, mboga, sigara kubwa, ndumu, msokoto, ganja, nk
Bangi iliyokaushwa, mbegu na misokoto
Bangi iliyosindikwa
Matumizi ya bangi huchochea matumizi ya dawa nyingine za kulevya kwa namna mbili; kwanza kwa kuchanganya bangi na dawa nyingine za kulevya au kwa kuhamia kwenye dawa zingine kama heroin na cocaine. Hali hii huongeza madhara kwa mtumiaji na hata wakati mwingine husababisha vifo.
Kilimo haramu cha bangi mara nyingi hufanyika kwenye vyanzo vya maji, misituni na milimani ambapo miti hukatwa au kuchomwa moto na kusababisha kutoweka kwa baadhi ya viumbe hai na uoto wa asili, kukauka kwa vyanzo vya maji, mmomonyoko wa udongo na hatimaye ukame. Uharibifu huu umejidhihirisha katika safu za milima ya Uluguru, Usambara, Udzungwa na maeneo ya Arumeru.
Kushamiri kwa kilimo haramu cha bangi, kunaweza kusababisha uhaba wa mazao ya chakula na hivyo kupelekea kupanda bei ya vyakula na hata janga la njaa.
Kutokana na athari za matumizi na kilimo haramu cha bangi, Taifa linaingia gharama kubwa katika kukabiliana na tatizo hili, ikiwemo utoaji wa elimu mashuleni na katika jamii, matibabu ya maradhi mbalimbali, uteketezaji mashamba na udhibiti wa biashara haramu ya bangi.
Bangi huchangia kuongezeka kwa umasikini kwa mtumiaji, jamii na taifa kwa ujumla na kupelekea kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Mafuta ya bangi
Sheria inasemaje kuhusu bangi?
Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, sura ya 95, kilimo na biashara ya bangi katika Taifa letu ni KOSA LA JINAI. Kwahiyo, kujihusisha kwa namna yoyote na bangi (kulima, kuuza, kuhifadhi, kutumia, kuichakata, nk) ni KOSA LA JINAI na adhabu yake inafikia hadi KIFUNGO CHA MAISHA JELA.
Utamsaidiaje mtumiaji wa bangi?
Mtumiaji anaweza kupunguza kiasi anachotumia taratibu na hatimaye kuacha.Aidha, asasi za kiraia huwasaidia watumiaji kuacha kwa kuwapa unasihi. Nyumba za upataji nafuu ‘sober house’ ambako hupitishwa kwenye hatua 12 za upataji nafuu. Kwa msaada zaidi tembelea tovuti www.dcea.go.tz
Ujumbe kwa jamii
Je, ni kweli bangi huongeza uwezo wa kusoma na kuelewa zaidi?
Hapana!. Bangi hufanya mishipa ya damu na ubongo kusinyaa, kunakosababisha kupungua kwa uwezo wa kufikiri na kumbukumbu. Kwa wanafunzi na vijana matumizi ya bangi hupunguza uwezo wao wa kufikiri, kusoma na kukumbuka na hii hupelekea kupata matokeo yasiyoridhisha katika masomo yao.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya
S.L.P 80327
8 Barabara ya Kivukoni Front, 11486 Dar es salaam
Dar es Salaam
Simu: +255 22 211 3754/57
Nukushi: +255 22 211 3752
Barua pepe: cg@dcea.go.tz
© 2023 Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya. Haki zote zimehifadhiwa..
Imesanifiwa, Imetengenezwa, na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) na Inaendeshwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya