Kanda ya Ziwa Yaendelea na Kampeni ya Uelimishaji Dhidi ya Dawa za Kulevya

Katika kuendeleza juhudi za taifa za kupambana na matumizi, biashara na usambazaji wa dawa za kulevya, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kupitia Ofisi ya Kanda ya Ziwa, imeendelea kutoa elimu kwa jamii mbalimbali katika mikoa ya Mara na Mwanza.
Mwezi Mei 2025, DCEA Kanda ya Ziwa imefanya kampeni maalum ya uelimishaji iliyoanzia katika shule za sekondari za Bomani, Mogabiri, Manga, Kibasuka, pamoja na shule za msingi na sekondari za Nkerege. Katika zoezi hilo, jumla ya wanafunzi zaidi ya 4,700 na walimu 100 walipatiwa elimu kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, hususan bangi na mirungi.
Maafisa wa DCEA walitoa uelewa juu ya namna ya kujiepusha na dawa hizo, pamoja na adhabu zinazotolewa kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa mtu yeyote atakayekutwa anazimiliki, kuzitumia au kuzisambaza.
Katika kijiji cha Nkerege, zaidi ya wananchi 300 pamoja na viongozi wa kijiji walishiriki kwenye kikao cha elimu. Wananchi walikiri kuwa hapo awali kilimo cha bangi kilikuwa kimeenea kwa kiwango kikubwa, lakini kutokana na juhudi za elimu na operesheni za DCEA, shughuli hiyo sasa imedorora. Waliomba mamlaka hiyo kufikisha elimu hiyo katika vijiji vingine ambavyo bado havijafikiwa.
Katika vijiji vya Nyarwana na Weigita, wananchi walihamasishwa kuunga mkono mapambano dhidi ya kilimo cha bangi. Serikali za vijiji hivyo zimeanzisha sheria ndogo za kijiji ili kudhibiti kilimo cha zao hilo haramu. Viongozi wa vijiji hivyo walituma salamu za pongezi kwa Kamishna Jenerali wa DCEA na kuahidi kuendelea kushirikiana na Mamlaka katika kulinda jamii dhidi ya dawa hizo.
Aidha, katika Wilaya ya Magu, DCEA ilitoa mafunzo kwa watendaji wa kata za Kisesa na Bujora pamoja na wenyeviti wa vijiji na vitongoji – jumla ya washiriki ikiwa 51. Mafunzo hayo yalilenga kuimarisha ulinzi na ushirikiano wa kijamii hasa baada ya kubainika kuwa baadhi ya maeneo ya Kisesa yanatumiwa kama njia ya usafirishaji wa dawa kutoka Mkoa wa Mara.
Kampeni hiyo ilihitimishwa kwa semina kwa madereva 60 wa bodaboda wa kata ya Kisesa. Semina hiyo ililenga kuwaelimisha juu ya hatari ya kubeba mizigo au abiria bila kujua wanachokisafirisha, jambo ambalo linaweza kuwaingiza katika matatizo ya kisheria iwapo litahusisha dawa za kulevya. DCEA iliwataka madereva hao kuwa makini na kushirikiana kwa karibu kwa kutoa taarifa za uhalifu.
Kampeni hii ya uelimishaji ya DCEA Kanda ya Ziwa ni mfano wa namna elimu ya kuzuia inaweza kuleta mabadiliko chanya kwa kushirikiana na jamii katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.