Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Khat

Mirungi ni aina ya dawa ya kulevya inayotokana na mmea unaoitwa “Catha edulis”. Mmea huo una kemikali za cathinone na cathine ambazo huongeza kasi ya utendaji wa mfumo wa fahamu. Mirungi ilikuwa inatumika tangu enzi za mababu kwenye nchi za pembe ya Afrika hususani Ethiopia, Eritrea, Kenya, Somalia pamoja na Rasi ya Arabuni nchini Yemen. Miru

ngi hutumika zaidi kwenye mikusanyiko ambayo hujumuisha zaidi wanaume ingawa katika miaka ya karibuni wanawake wamejiingiza katika matumizi. Nchini kwetu mirungi hustawi na hupatikana kwa wingi katika mikoa ya Kilimanjaro- Same, Tanga- Lushoto na Arusha Mlima Meru. Kiasi kingi cha mirungi huingizwa nchini isivyo halali kutoka nchi jirani ya Kenya ambako ni zao halali la biashara. Mirungi hufahamika kwa majina ya gomba, veve, miraa, kangeta, mkokaa, colombo, asili, mbaga, alenle, nk.

MADHARA YA MIRUNGI

 • Huongeza kasi ya mapigo ya moyo hivyo kuweza kuongeza shinikizo la damu, kiharusi na hata kusababisha kifo.
 • Husababisha vidonda vya utumbo mdogo, saratani ya mdomo, koo na tumbo
 • Husababisha upungufu wa msukumo wa kufanya tendo la ndoa, kumaliza haraka na kutoweza kudumu kwenye tendo la ndoa kwa muda mrefu
 • Hupunguza ubora wa mbegu za kiume na kuvuruga mfumo wa utokaji wake na hata kusababisha ugumba
 • Mtumiaji hukosa usingizi na ulevi ukiisha mwilini husababisha usingizi mzito unaoweza kusababisha ajali hasa kwa madereva
 • Huchochea ukatili, fujo, ugomvi, kuongea sana masuala ya kusadikika na kuhangaika.
 • Mtumiaji hukosa kabisa hamu ya kula na kupungua uzito.
 • Mirungi husababisha upungufu wa maji mwilini na kuleta tatizo la kukosa choo pamoja na ugonjwa wa bawasiri
 • Mtumiaji mirungi akiikosa mirungi hupata uchovu, sonona, hasira za ghafla, kutetemeka, kushindwa kutulia na njozi za kutisha (night mares)
 • Utumiaji mirungi huozesha meno na yale yanayosalia hubadilika rangi, fizi kuuma na harufu ya mdomo.
 • Mirungi huharibu ufanisi wa ini mwilini katika kuchuja sumu za mwili
 • Mirungi huamsha magonjwa ya akili yanayojitokeza kwa vipindi “mwezi mchanga” kwa watumiaji wenye tatizo hilo
 • Wanawake wanaotumia mirungi kipindi cha ujauzito wana hatari ya kupata maumivu ya kifua, kuongezeka kwa mapigo ya moyo na msukumo wa damu
 • Matumizi ya mirungi yanaweza kusababisha kuzaliwa kwa watoto wenye uzito mdogo ambao huweza kukataa kunyonya kutokana na ladha ya maziwa kubadilishwa na viuatilifu vinavyotumika kwenye kilimo cha mirungi
 • Watumiaji mirungi hujikuta wakipenda kuvuta sigara au kunywa pombe wanapokosa usingizi hivyo kudhuru zaidi afya zao.
 • Mtumiaji wa mirungi hutumia fedha ambazo zingekidhi mahitaji ya familia kununulia mirungi hivyo kusababisha migogoro
 • Utafunaji mirungi hutumia muda mwingi na hufanyika muda wa kazi au muda ambao mtumiaji hutakiwa kujumuika na familia yake hivyo kushusha uzalishaji na ukaribu wa familia.

Sheria inasemaje kuhusu mirungi?

Mirungi katika taifa letu ni haramu.

Kujihusisha kwa namna yoyote na mirungi (kulima, kuuza, kuhifadhi, kutumia, nk)ni KOSA LA JINAI na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha maisha

Baadhi ya nchi za Ulaya ambazo awali ziliruhusu matumizi ya mirungi zimeanza kuiharamisha baada ya kuona madhara yake

Utamsaidiaje mtumiaji wa mirungi

Mtumiaji anaweza kupunguza kiasi anachotumia taratibu na hatimaye kuacha.Aidha, asasi za kiraia huwasaidia watumiaji kuacha kwa kuwapa unasihi. Nyumba za upataji nafuu ‘sober house’ ambako hupitishwa kwenye hatua 12 za upataji nafuu. Kwa msaada zaidi tembelea tovuti www.dcea.go.tz

Ujumbe kwa jamii

 • Mirungi HAIONGEZI ufanisi kazini, ufaulu katika masomo, udereva wala nguvu za kiume
 • Wazazi na walezi wawalee watoto katika maadili mema ikiwemo kuwa nao karibu na kuwasikiliza
 • Vijana wajifunze na kuzingatia stadi za maisha
 • Epuka kutumia dawa za kulevya pamoja na kujiepusha na makundi hatarishi yanayoweza kukuingiza kwenye utumiaji