Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Cocaine

J

COCAINE NI NINI?

Ni dawa ya kulevya inayotokana na majani ya mmea unaojulikana kitaalam kama erythroxylum coca ambao hulimwa zaidi kwenye nchi ya Colombia ikifuatiwa na Peru na Bolivia. Asili ya dawa hii ni kuongeza kasi ya utendaji wa mfumo wa fahamu. Watumiaji hutumia cocaine kwa njia ya kunusa, kuvuta, kujidunga au kupaka ambapo huathirika na kuwa wateja wa dawa hiyo. Cocaine huwa katika hali ya unga mweupe au vijiwe vyeupe. Majina maarufu ya dawa hii yanayotumika mitaani ni pamoja na pele, diego, white sugar na sembe.

Unga wa cocaine na heroin huweza kufanana ingawa heroin hupatikana zaidi kuliko cocaine hapa nchini.

J

ATHARI ZA COCAINE

Kiafya:

  • Hufanya mishipa ya damu kusinyaa na kuongeza msukumo la damu na mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio hivyo kuleta shinikizo la damu, shambulizi la moyo, kiharusi au kifo cha ghafla
  • Huleta matatizo ya kiakili kama kujihisi unataka kudhuriwa, hasira, ukatili, vurugu, kukosa utulivu na kutaka kujiua.
  • Cocaine ikitumika kwa njia ya kunusa husababisha uwezo wa kunusa kupotea, pua kutoboka, mafua yasiyopona na kutoka damu puani .
  • Uvutaji wa cocaine ya mawe huharibu mapafu na kupata kikohozi kikali pamoja na kupumua kwa shida
  • Cocaine husababisha kusinyaa kwa mishipa ya damu kwenye mfumo wa chakula na utumbo kuoza
  • Cocaine huozesha meno kutokana na ongezeko la asidi na ukavu wa mdomo
  • §Hatari ya maambukizi ya homa ya ini, VVU na kifua kikuu kutokana na kushirikiana sindano, kubakwa, biashara ya ngono, kushiriki ngono zembe, kuishi mazingira yasiyo na hewa safi, nk.
  • Cocaine inapokosekana arosto hutokea na kupata uchovu mkali, usingizi, kutetemeka, kuhisi kutambaliwa na vitu mwilini, kutapika, kuwa dhaifu na kushindwa kuwa na utulivu. Arosto pia husababisha kukosa furaha, maumivu makali, kuharisha, homa, kukosa umakini na kuwa na hamu kubwa ya kutumia cocaine
  • Huweza kusababisha vifo kutokana na kuzidisha kiasi cha matumizi
  • Cocaine ikichanganywa na pombe huweza kusababisha kifo.
  • Kukosa usingizi na kuweza kusababisha ajali
  • Kukosa hamu ya kula na kusababisha afya kudhoofu
  • Utumiaji cocaine huchochea uvutaji wa sigara wa mfululizo

Kijamii

  • Mtumiaji kutowajibika na kushindwa kutimiza majukumu katika familia na kusababisha kuvunjika kwa ndoa, kutelekeza watoto na kwa watoto hufukuzwa na kuishi kwenye mageto
  • Ongezeko la vitendo vya uhalifu vikiwemo udokozi, unyang’anyi, utapeli pamoja na mmomonyoko wa maadili (biashara ya ngono).
  • Biashara ya dawa za kulevya huambatana na uhalifu mkubwa kwenye jamiikama ujangili, biashara ya binadamu, biashara haramu ya silaha, money laundering, utekaji, ugaidi, madanguro, nk

Kiuchumi

  • Matumizi ya dawa za kulevya hupunguza nguvu kazi ya taifa na kuongeza umasikini kwa familia na jamii kwa ujumla.
  • Biashara ya dawa za kulevya husababisha mzunguko wa fedha haramu, mfumuko wa bei, utakatishaji fedha, kukithiri kwa rushwa na kuongeza tofauti ya kipato
  • Serikali hutumia gharama kubwa kudhibiti tatizo la dawa za kulevya kwenye ukamataji, matibabu, kutoa elimu, nk

Wanafunzi wengi wanaotumia cocaine hushindwa kuzingatia masomo yao na wengine kushindwa kumaliza shule. Vijana hawa hujikuta hawakubaliki katika jamii zao na kunyanyapaliwa hivyo hujiunga na magenge ya wahalifu.

    Cocacola na cocaine

    Kwenye miaka ya 1886 kinywaji cha Coca-Cola kilipoanzishwa kilikuwa na kiasi kidogo cha cocaine. Baada ya madhara ya cocaine kudhihirika katika jamii iliondolewa kwenye Coca-Cola mwaka 1903.

    Sheria inasemaje kuhusu cocaine?

    Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, sura ya 95, kujihusisha na cocaine kwa namna yoyote katika taifa letu ni KOSA LA JINAI. Kwahiyo, kusafirisha ndani na nje ya nchi, kuuza, kuhifadhi, kusambaza, kutumia na kutengeneza cocaine ni KOSA LA JINAI na adhabu yake inafikia hadi KIFUNGO CHA MAISHA JELA.

    J

    Utamsaidiaje mtumiaji wa cocaine

    Mtumiaji anaweza kupunguza kiasi anachotumia taratibu na hatimaye kuacha.Aidha, asasi za kiraia huwasaidia watumiaji kuacha kwa kuwapa unasihi. Nyumba za upataji nafuu ‘sober house’ ambako hupitishwa kwenye hatua 12 za upataji nafuu. Kwa msaada zaidi tembelea tovuti www.dcea.go.tz

    Ujumbe kwa jamii

    1.Wazazi na walezi wawalee watoto katika maadili mema ikiwemo kuwa nao karibu na kuwasikiliza

    2.Vijana wajitambue na kujiepusha na makundi hatarishi yanayoweza kuwaingiza kwenye utumiaji wa sigara, ugoro, pombe, shisha au bangi ambavyo watumiaji wengi wa cocaine wanakiri walianza navyo

    3.Usijaribu kuonja cocaine kwani inaleta uraibu (uteja) kwa haraka na ni vigumu sana kuachana nayo.

    4.Watumiaji wasinyanyapaliwe waelekezwe kwenye tiba