Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA Yazuia Uingizwaji wa Tani 14 za Kemikali Bashirifu, Kilo 4,500 za dawa za kulevya zakamatwa

Imewekwa: 05 May, 2025
DCEA Yazuia Uingizwaji wa Tani 14 za Kemikali Bashirifu,  Kilo 4,500 za dawa za kulevya zakamatwa

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kuzuia uingizwaji wa tani 14 za kemikali bashirifu na kukamata kiasi kikubwa cha dawa za kulevya katika operesheni zilizofanyika katika mikoa sita nchini, hatua inayodhibiti athari kubwa za kiafya na kijamii.

Akizungumza na vyombo vya habari tarehe 23 Aprili 2025, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema kuwa operesheni hizo zilizofanyika kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola zimefanikisha ukamataji wa kilogramu 4,568 za dawa za kulevya, kuteketeza ekari 178 za mashamba ya bangi na kushikilia magari saba, pikipiki tano na bajaji moja zilizotumika katika uhalifu huo. Aidha, jumla ya watuhumiwa 35 wanashikiliwa kuhusiana na matukio hayo.

Katika mafanikio ya kipekee, DCEA kwa kushirikiana na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (INCB) na mamlaka nyingine za kimataifa, ilifanikiwa kuzuia kilogramu 4,000 za kemikali aina ya 1-Boc-4-piperidone na kilogramu 10,000 za acetic anhydride kutoka bara la Asia ambazo zilikuwa zikiingizwa bila vielelezo halali. Kemikali hizo zingetumika kutengeneza dawa hatari kama fentanyl, heroin, methaqualone na mandrax.

Kamishna Lyimo alieleza kuwa kiasi hicho cha 1-Boc-4-piperidone kingeweza kuzalisha kilo 8,000 za fentanyl — kiwango kinachoweza kusababisha vifo kwa watu bilioni nne endapo kingeingia sokoni. “Kilogramu moja ya fentanyl inaweza kuua watu 500,000 kulingana na afya na historia ya mtumiaji,” alibainisha.

Katika tukio jingine mkoani Mbeya, raia wa Uganda Herbert Kawalya alikamatwa akiwa na pakti 10 za pipi zenye bangi yenye viwango vya juu vya kemikali hatari ya THC (asilimia 92), akiwa anasafirisha kwa gari aina ya Mercedes Benz kutoka Uganda. Taarifa hiyo inaonesha namna wahalifu wanavyozidi kutumia mbinu fiche katika kuingiza dawa hizo nchini.

Operesheni nyingine ziliendelea mkoani Mbeya ambako kilo 1,658 za skanka na kilo 128.7 za bangi zilikamatwa kutoka Malawi. Katika jiji la Dar es Salaam, kilo 220.67 za skanka zilifichwa chooni Chanika huku kilo 11 zikiwa bandarini zikielekea Zanzibar.

Aidha, kilo 733.74 za methamphetamine, kilo 91.62 za heroin, kilo 692.84 za mirungi na kilo 115.05 za bangi zilikamatwa katika mikoa ya Arusha, Tanga na Manyara, pamoja na kuteketezwa kwa ekari mbili za mashamba ya bangi. Mkoani Tabora, ekari 176 za mashamba ya bangi ziliteketezwa na kilo 845 za bangi kukamatwa, huku kilo 98.35 za bangi zikikamatwa Kahama na Shinyanga.

DCEA imeeleza kuwa juhudi hizi zimeokoa maisha ya maelfu ya Watanzania, hasa vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa. Kamishna Lyimo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Mamlaka kwa kutoa taarifa mapema kupitia namba 119, na kwa wazazi kufuatilia mwenendo wa watoto wao.

Pia, kampuni zinazotumia kemikali viwandani na kwenye kilimo zimekumbushwa kuzingatia sheria na kuepuka kushirikiana na magenge ya kihalifu.