Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Heroin

J

HEROIN NI NINI?

Ni aina ya dawa ya kulevya inayotengenezwa na kemikali ya asili inayoitwa ‘morphine’ ambayo inapatikana kwenye utomvu ‘opium’ wa tunda la mmea wa afyuni ‘opium poppy’ unaolimwa zaidi kwenye nchi za Afghanstan, Myanmar na Laos. Hapa nchini, heroin inashika nafasi ya pili kwa matumizi baada ya bangi, na inatumiwa kwa njia ya kuvuta ikiwa imechanganywa na kiasi kidogo cha bangi na sigara au kwa njia ya kunusa na kujidunga. Heroin ni kati ya dawa za kulevya zinazoongoza kwa kusababisha uteja haraka, vifo vinavyotokana na kuzidisha kiasi cha matumizi au maradhi mbalimbali, pia ni dawa ambayo ina watumiaji wengi wanaohitaji tiba. Heroin hujulikana kwa majina ya mtaani kama unga, ngada, teli (cocktail), msharafu, white, kijiwe, brown, nk.

Utomvu ukivunwa kwenye mmea wa afyuni (opium)

J

MADHARA YA HEROIN

Kiafya

 • Husababisha magonjwa ya moyo, ini, mapafu, meno, ngozi, figo na saratani
 • Mazingira duni ya utumiaji na kushirikiana vifaa husababisha maambukizi ya kifua kikuu, VVU na homa ya ini
 • Matumizi ya heroin na pombe huweza kusababisha kifo
 • Mtumiaji anapoacha kutumia heroin hupatwa na arosto inayoambatana na dalili zifuatazo maumivu makali, homa, kuharisha, kizunguzungu na kichefuchefu
 • Heroin hupunguza kasi ya utendaji kazi wa mfumo wa fahamu na kuathiri umakini, hivyo kusababisha ajali au kushiriki ngono zembe.
 • Kukosa hamu ya kula na kudhoofu kiafya
 • Upungufu wa maji mwilini kunakosabisha kukosa choo
 • Kujidunga husababisha mishipa ya damu kusinyaa au kupotea na hivyo kushindwa kupata msaada wa matibabu kwa haraka inapohitajika
 • Huweza kusababisha vifo kutokana na kuzidisha kiasi cha matumizi

Kijamii

 • Mtumiaji kutowajibika na kushindwa kutimiza majukumu katika familia na kusababisha kuvunjika kwa ndoa, kutelekeza watoto na kwa watoto hufukuzwa na kuishi kwenye mageto
 • Ongezeko la vitendo vya uhalifu vikiwemo udokozi, unyang’anyi, utapeli pamoja na mmomonyoko wa maadili (biashara ya ngono).
 • Biashara ya heroin imesababisha vijana wa kitanzania kuwekwa rehani nje ya nchi (bondi) na kuhatarisha maisha yao na taswira ya nchi.
 • Biashara ya dawa za kulevya huambatana na uhalifu mkubwa kwenye jamiikama ujangili, biashara ya binadamu, biashara haramu ya silaha, money laundering, utekaji, ugaidi, madanguro, nk

Kiuchumi

 • Matumizi ya dawa za kulevya hupunguza nguvu kazi ya taifa na kuongeza umasikini kwa familia na jamii kwa ujumla.
 • Biashara ya dawa za kulevya husababisha mzunguko wa fedha haramu, mfumuko wa bei, utakatishaji fedha, kukithiri kwa rushwa na kuongeza tofauti ya kipato
 • Serikali hutumia gharama kubwa kudhibiti tatizo la dawa za kulevya kwenye ukamataji, matibabu, kutoa elimu, nk

Kwa wanawake

 • Huweza kuharibu mimba au kuzaa watoto njiti.
 • Huzaa watoto wenye uteja na heroin
 • Watoto wanaozaliwa hudumaa kimwili na kiakili na mara nyingi hufariki kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano

Wanafunzi

Wengi wanaotumia heroin hushindwa kuzingatia masomo yao na wengine kushindwa kumaliza shule. Vijana hawa hujikuta hawakubaliki katika jamii zao na kunyanyapaliwa hivyo hujiunga na magenge ya wahalifu.

Sheria inasemaje ukijihusisha na heroin?

Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, sura ya 95, kujihusisha na heroin kwa namna yoyote katika taifa letu ni KOSA LA JINAI. Kwahiyo, kusafirisha ndani na nje ya nchi, kuuza, kuhifadhi, kusambaza, kutumia na kutengeneza heroin ni KOSA LA JINAI na adhabu yake inafikia hadi KIFUNGO CHA MAISHA JELA.

t

Utamsaidiaje mtumiaji wa heroin?

Mtumiaji anaweza kupunguza kiasi anachotumia taratibu na hatimaye kuacha.Wanaweza kupatiwa tiba ya methadone inayopatikana kwenye baadhi ya vituo vya afya. Aidha, asasi za kiraia huwasaidia watumiaji kuacha kwa kuwapa unasihi na huduma nyingine. Vilevile, nyumba za upataji nafuu ‘sober house’ huwasaidia kwa kuwapitisha kwenye hatua 12 za upataji nafuu.

Ujumbe kwa jamii

 1. Wazazi na walezi wawalee watoto katika maadili mema ikiwemo kuwa nao karibu na kuwasikiliza
 2. Vijana wajitambue na kujiepusha na makundi hatarishi yanayoweza kuwaingiza kwenye utumiaji wa sigara, ugoro, pombe, shisha au bangi ambavyo watumiaji wengi wa heroin wanakiri walianza navyo.
 3. Usijaribu kuonja heroin kwani inaleta uraibu (uteja) kwa haraka na ni vigumu sana kuachana nayo.
 4. Watumiaji wasinyanyapaliwe waelekezwe kwenye tiba