Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Zaidi ya tani mbili na nusu za dawa za kulevya zateketezwa

Imewekwa: 29 December, 2022
Zaidi ya tani mbili na nusu za dawa za  kulevya zateketezwa

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeshirikiana na wadau wengine muhimu kutoka Taasisi mbalimbali kuteteteza zaidi ya tani mbili na nusu za dawa za kulevya zilizohusisha mashauri ya kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2022. Veronica Matikila akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Kamisha Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Kusaya amesema, uteketezaji huu uliofanyika katika kiwanda cha saruji cha Twiga Wazo jijini Dar es salaam, ni wa kawaida na hufanyika pale mashauri ya dawa za kulevya yanapomalizika mahakamani.

"Uteketezaji huu wa dawa za kulevya umefanyika kufuatia kumalizika kwa mashauri ya dawa za kulevya katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mahakama ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, na Mahakama za Hakimu Mkazi za Kisutu na Kibaha Pwani pamoja na Mahakama za Wilaya ya Kinondoni, Ilala, Temeke na Kigamboni" amesema Matikila.

Miongoni mwa dawa za kulevya zilizoteketezwa ni heroin kilo 569.25, kilo 15.3 za cocaine na tani mbili za bangi na mirungi.

Aidha, amesema hii ni mara ya pili kwa mwaka 2022 uteketezaji wa dawa za kulevya kufanyika. Uteketezaji wa kwanza ulifanyika mwezi Februari ambapo jumla ya kilo 250.7 ziliteketezwa katika kiwanda cha Saruji cha Dangote mkoani Mtwara. Kwa mwaka 2021, uteketezaji ulifanyika mkoani Mtwara ukihusisha kilo 355 za dawa za kulevya aina ya Methamphetamine. Pia, hekari 41 za mashamba ya bangi na mirungi ziliteketezwa katika mikoa ya Pwani, Arusha na Kilimanjaro.

Matikila ameongeza kuwa, hii ni mara ya tatu kufanya uteketezaji katika kiwanda hiki cha Twiga tangu kuanzishwa kwa Mamlaka mwaka 2017. Mara ya kwanza uteketezaji ulifanyika tarehe 8 Oktoba, 2019 ambapo kilo 120.91 za heroin, kilo 70.96 za cocaine ziliteketezwa. Mara ya pili ulifanyika tarehe 12 Novemba, 2020 ambapo kilo 118.174 za heroin, kilo 3.932 za cocaine na kilo 120 za bangi ziliteketezwa.

Amefafanua kwamba, uteketezaji wa dawa za kulevya hufanyika kwa namna ambayo hulinda afya na kuzingatia kanuni za utunzaji wa mazingira huku ukishuhudiwa na wadau muhimu. “Wadau hao ni Hakimu au Jaji, Kamishna Jenerali, Inspekta Jenerali wa Polisi, Mkurugenzi wa Mashtaka, Mkemia Mkuu wa Serikali, Idara ya Usalama wa Taifa, Baraza la Taifa la Mazingira na wadau wengine watakaoalikwa na Kamishna Jenerali” amefafanua Matikila.

Kipekee amewashukuru Majaji na Mahakimu, Inspekta Jenerali wa Polisi, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini, Mkemia Mkuu wa Serikali, Idara ya Usalama wa Taifa, Baraza la Taifa la Mazingira, Waandishi wa Habari na wadau wengine walioshiriki katika kufanikisha zoezi hili muhimu la uteketezaji pamoja na mwekezaji wa Kiwanda cha Saruji cha Twiga kwa kuendelea kutoa ushirikiano na kuruhusu zoezi hili kufanyika kiwandani kwake.