Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA Yatoa Elimu kwa Jamii kuhusu Dawa za Kulevya kupitia Maonesho ya Sabasaba

Imewekwa: 14 July, 2026
DCEA Yatoa Elimu kwa Jamii kuhusu Dawa za Kulevya kupitia Maonesho ya Sabasaba

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imetumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, mbinu zinazotumiwa katika biashara haramu ya dawa hizo na wajibu wa jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya tatizo hilo.

Kupitia mabanda yake yaliyokuwa katika Viwanja vya Maonesho ya Sabasaba na katika banda la Ofisi ya Waziri Mkuu, DCEA iliwafikia maelfu ya wananchi kwa kutoa elimu kupitia vipeperushi na machapisho mbalimbali, maonesho ya sampuli za dawa za kulevya na kemikali bashirifu, huku wataalamu wakitoa elimu,  ufafanuzi na kujibu maswali mbalimbali.

Akizungumza wakati wa maonesho hayo, Afisa Elimu kwa Umma wa DCEA, Shaban Miraji, alisema maonesho hayo yameendelea kuwa fursa muhimu ya kuifikia jamii na kuongeza uelewa kuhusu tatizo la dawa za kulevya.

"Wananchi wengi husikia majina ya dawa za kulevya lakini hawajawahi kuziona. Kupitia maonesho haya wamepata nafasi ya kuzitambua na kujifunza madhara yake, jambo litakalowasaidia kuchukua hatua mapema wanapokutana nazo katika mazingira yao," alisema Miraji.

Miraji aliongeza kuwa elimu hiyo imelenga makundi yote ya jamii, hususan vijana, ili kuwajengea uelewa utakaowawezesha kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na kushiriki kikamilifu katika kuzuia na kupambana na tatizo hilo.

Maonesho hayo pia yalipata kutembelewa na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas James Lyimo, ambaye alijionea huduma zinazotolewa katika mabanda ya taasisi mbalimbali zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Akiwa katika ziara hiyo, Kamishna Jenerali alipata fursa ya kujionea huduma na shughuli zinazotekelezwa na taasisi mbalimbali zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, zikiwemo Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Wakala wa Kazi Tanzania (TaESA), Wakala wa Huduma za Uchapishaji Serikalini (GPSA), Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali (Government Printer), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Tume ya Ushindani (FCC), pamoja na taasisi nyingine zinazotoa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi, kubadilishana uzoefu na kujionea namna taasisi hizo zinavyowasilisha huduma kwa wananchi kupitia maonesho hayo.

Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), DCEA imeendelea kuimarisha juhudi za kuelimisha umma kuhusu madhara ya dawa za kulevya, kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya tatizo hilo na kuunga mkono jitihada za Serikali za kujenga jamii salama, yenye afya na maendeleo endelevu.