Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA, ZDCEA Zaungana Kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya 2026

Imewekwa: 14 July, 2026
DCEA, ZDCEA Zaungana Kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya 2026

Tarehe 26 Juni ya kila mwaka, mataifa mbalimbali duniani huadhimisha Siku ya Kimataifa dhidi ya Matumizi Mabaya na Usafirishaji Haramu wa Dawa za Kulevya. Maadhimisho haya yalianzishwa na Umoja wa Mataifa kwa lengo la kutoa fursa kwa nchi wanachama kutafakari kwa pamoja na kuimarisha juhudi za kukabiliana na changamoto ya dawa za kulevya, ambayo inaendelea kuathiri afya ya jamii, usalama, uchumi na maendeleo ya kijamii.

Tanzania, ikiwa ni miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, huungana na jumuiya ya kimataifa kuadhimisha siku hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kupitia shughuli za uelimishaji, uhamasishaji na utekelezaji wa mikakati ya kuzuia na kudhibiti matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.

Mabadiliko ya mifumo ya usafirishaji, mbinu mpya za usambazaji na kuibuka kwa aina mbalimbali za dawa za kulevya yameongeza ugumu katika kukabiliana na tatizo hili. Kutokana na hali hiyo, mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji mbinu bunifu, shirikishi na zinazozingatia mazingira halisi ya jamii.

Katika kuakisi hitaji hilo, maadhimisho ya mwaka 2026 yamebebwa na kaulimbiu isemayo:“Ubunifu wa Kimkakati: Suluhisho la Changamoto ya Dawa za Kulevya.”

Kaulimbiu hii inasisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia, maarifa mapya, ushirikiano wa wadau na mikakati madhubuti katika kuzuia, kudhibiti na kutafuta suluhisho endelevu dhidi ya changamoto ya dawa za kulevya.

Nchini Tanzania, maadhimisho ya mwaka 2026 yalilenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na kuimarisha ushirikiano wa wadau katika kubuni mikakati endelevu ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Katika kuunga mkono maadhimisho hayo, shughuli mbalimbali za kijamii, kampeni za uelimishaji na maonesho ya kutoa elimu zilifanyika katika maeneo mbalimbali nchini kupitia ofisi za kanda za Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA). Shughuli hizo zilitoa fursa kwa wananchi kupata uelewa mpana kuhusu madhara ya dawa za kulevya na umuhimu wa ushiriki wa pamoja katika kukabiliana na tatizo hilo.

Aidha, maadhimisho hayo yalisisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni jukumu la kila mmoja. Wazazi, walezi, walimu, viongozi wa jamii, wataalamu wa afya, vijana na wadau wengine wana nafasi muhimu katika kuzuia kuenea kwa matumizi mabaya ya dawa za kulevya.

Jamii ilihimizwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya uhalifu vinavyohusiana na dawa za kulevya, kuimarisha malezi bora na kuwasaidia waathirika kupata huduma za matibabu, ushauri nasaha na urekebishaji tabia.

Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa dhidi ya Matumizi Mabaya na Usafirishaji Haramu wa Dawa za Kulevya mwaka 2026 kilifanyika Zanzibar, ambapo Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA) waliungana kuhitimisha maadhimisho hayo.

Mgeni rasmi katika kilele hicho alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambaye aliwakilishwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.

Maadhimisho hayo yameendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kitaifa na kimataifa, pamoja na matumizi ya ubunifu wa kimkakati katika kujenga mifumo madhubuti ya kukabiliana na changamoto ya dawa za kulevya na kulinda afya na usalama wa jamii.