Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Matumizi ya Gundi na Dawa Tiba Zenye Asili ya Kulevya Changamoto Mpya Katika Udhibiti wa Dawa za Kulevya Nchini

Imewekwa: 03 July, 2020
Matumizi ya Gundi na Dawa Tiba Zenye Asili ya Kulevya Changamoto Mpya Katika Udhibiti wa Dawa za Kulevya Nchini

Baada ya udhibiti wa dawa za kulevya kuwa mkubwa nchini, Mamlaka inakumbana na changamoto mpya ya matumizi ya gundi na dawa tiba zenye asili ya kulevya kama njia mbadala ya dawa za kulevya.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana, Sera na Watu wenye ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika siku ya maadhimisho ya kupiga vita dawa za kulevya duniani ambayo hufanyika kila ifikapo tarehe 26 Juni kila mwaka.

Katika mkutano huo, Waziri Jenista alisema tatizo la dawa za kulevya katika jamii ni mtambuka linalohitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kupambana nalo. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inatekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na Wizara mbalimbali, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, na Taasisi nyingine za Serikali na zisizo za Serikali pamoja na Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa.

Kwa mwaka 2015-2020, Mamlaka imetekeleza kazi mbalimbali katika kukabiliana na dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2017, ambapo maboresho hayo yameweka sheria kali zaidi kwa watakaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Pia Mamlaka inaendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya, ambapo kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu imeweza kuanzisha vilabu vya kupinga matumizi ya dawa za kulevya katika shule za msingi, sekondari na vyuoni.

“Vile vile, elimu bora kuhusu tatizo la dawa za kulevya imekuwa ikitolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari kama vile televisheni, magazeti, warsha za kitaifa na makongamano pamoja na mitandao ya kijamii kuhusu madhara ya dawa hizo pamoja na udhibiti wa uchepushwaji wa kemikali bashirifu. Hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia wimbi la vijana kuingia kwenye matumizi na biashara ya dawa hizo,” alisema waziri.

“Pia tumefanikiwa kubaini na kuvunja mitandao mikubwa ya dawa za kulevya nchini. Mamlaka kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za kimataifa kama vile UNODC, Interpol, DEA, CIA na NCA imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhoofisha na kuvunja mitandao mikubwa ya wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi, Kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2019 ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Tanzania ilifanikiwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya kwa 90% na imeshinda kesi kubwa za wafanya biashara wakubwa wa dawa za kulevya” alisema.

Kutokana na udhibiti huo, watumiaji wamejielekeza kwenye matumizi ya bangi, mirungi, gundi na dawa tiba zenye asili ya kulevya, jambo ambalo kwa sasa Serikali inajipanga kupanua wigo wa kulishughulikia na kulidhibiti.

“Matumizi ya gundi ni eneo ambalo limewekewa mkakati maalumu; tumegundua watoto wanatumia, kimsingi tunaangalia uwezekano wa kuweka utaratibu ili matumizi ya gundi yadhibitiwe na isitumike kinyume. Kama tunavyojua gundi hutumika kwenye mambo mbalimbali lakini wengine wanatumia kama kilevi,” alisema.

Kuhusu dawa tiba, Mhagama alisema serikali Kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamabana na Dawa za Kulevya imejipanga kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ili kudhibiti matumizi yake kama ambavyo sheria imeweka utaratibu wa wizara hiyo kusimamia dawa hizo. Alisema kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015 hadi Juni 2020, dawa za kulevya aina ya; bangi kilo 188,489.93, mirungi kilo 124,080.33, cocaine kilo 58.46 na heroin kilo 635.57 zimekamatwa.

“ Katika ukamataji huo, jumla ya watuhumiwa 73,920 walikamatwa, pia Mamlaka imefanikiwa kufanya ukaguzi katika Makampuni 167 yanayojihusisha na uingizaji wa kemikali bashirifu na kukamata kiasi cha lita za ujazo 480,000 na kilo 22,145 za kemikali bashirifu zilizoingia nchini bila ya kufuata utaratibu,”alisema.

Kuhusu upanuzi wa huduma za tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya, Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Taasisi nyingine zisizo za kiserikali imefanikiwa kupanua huduma za tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya nchini, ambapo hadi sasa tuna vituo nane (8) nchini ambavyo vinahudumia waathirika kila siku.