Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Matumizi ya Dawa za Tiba kama mbadala wa Dawa za Kulevya

Imewekwa: 30 September, 2019
Matumizi ya Dawa za Tiba kama mbadala wa Dawa za Kulevya

Baada ya udhibiti wa Dawa za Kulevya kuwa mkubwa upatikaji wa dawa hizo umekuwa mgumu, zinapatikana kwa uchache na kwa kificho sana. Hali hiyo imesababisha watumiaji wa dawa hizo kugeukia kwenye matumizi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya kama vile Pethidine, Valium, Morphine na Tramadol na nyingine nyingi .

Dawa hizi hutumika hospitali kwa matibabu ya magonjwa mbalimbali, lakini waraibu wa dawa za kulevya wanapokosa kosa dawa za kulevya wanageukia dawa hizi kama mbadala wa dawa za kulevya kwasababu inaaminika kuwa dawa hizi zinapotumika kinyume na ushauri wa madaktari zinaweza kuleta matokea sawa na dawa za kulevya.

Akizungumzia athari za matumizi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya kama mbadala wa dawa za kulevya, kamishna wa kinga na tiba wa mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya Dkt. Peter Mfisi amesema, athari za matumizi ya dawa hizi zinamlenga mtumiaji moja kwa moja na jamii kwa ujumla.

``hawa watu wanaotumia dawa tiba zenye asili ya kulevya hulazimika kubadili dozi ya kawaida inayotolewa na daktari na kuifanya ya juu zaidi. Mfano dawa aina ya tramadol inayotumika kutibu maumivu dozi yake ni kati 50mg hadi 100mg ambapo mgonjwa atatumia kati ya mara 2 hadi mara 3 kwa siku kwa muda maalumu. Ila sasa watumiaji wa dawa hizo kwa kujifurahisha wanaweza wakatumia kati ya 500mg hadi 1000mg kwa siku na matumizi haya yanachukua muda mrefu zaidi “

Akiendelea kuzungumza, Dkt Mfisi amesema kwamba matumizi ya dozi kubwa kwa muda mrefu huweza kuleta madhara makubwa katika miili yao ikiwepo magonjwa ya figo, ini, pamoja na uraibu wa dawa hizo.

Wakati katika jamii, huweza kusababisha uhaba wa dawa husika au kutokupatikana kwenye mzunguko wa matibabu kutokana na waraibu hawa kutumia kiwango kikubwa cha dawa kwa wakati mmoja na kwa muda mrefu hivyo kupelekea jamii kuathirika .

Akizungumzia namna dawa hizi zinavyowafikia watu Dkt. Mfisi amesema “dawa hizi zinawafikia watu kutokana na baadhi ya wahudumu wa afya wenye dhamana ya kutunza dawa hizi kuzitoa kiholela. Aidha dawa hizi zimekuwa ikiuzwa kwenye maduka ya dawa bila kuwepo na cheti cha daktari kama inavyotakiwa hivyo kusababisha dawa hizo kuwafikia waraibu kwa ukaribu, Pia baadhi ya wafanya biashara wamekuwa wakiziingiza nchini bila kibali maalumu”.

Katika kutatua changamoto hii, Mamlaka ya udhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na bohari ya dawa , bodi ya famasia, Mamlaka ya dawa na vifaa tiba pamoja na maabala ya mkemia mkuu wa serikal wamefanya mawasiliano kuongeza udhibiti wa dawa hizi ili zisipatikane kiholela.