Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA inashiriki Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2025 Jijini Mbeya

Imewekwa: 11 October, 2025
DCEA inashiriki Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2025 Jijini Mbeya

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inashiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Uhindini jijini Mbeya. Maadhimisho haya, ambayo hufanyika kila mwaka, yanalenga kuwaunganisha vijana ili kubadilishana uzoefu, kujifunza, na kutambua fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii zinazoweza kuwainua kimaendeleo.

Maadhimisho haya yanaenda sambamba na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na Siku ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambayo huadhimishwa Oktoba 14 kila mwaka.

Kupitia ushiriki wake katika maonesho haya, DCEA imeweka banda maalum linalotoa elimu kwa umma kuhusu madhara yatokanayo na matumizi na biashara ya dawa za kulevya, sambamba na kuhamasisha vijana kujiepusha na vishawishi vya kuingia katika matumizi na biashara ya dawa hizo.

Wananchi na wadau mbalimbali wameendelea kujitokeza kwa wingi kutembelea banda la DCEA ambapo wanaelimishwa  Pamoja na kuona sampuli halisi za dawa za kulevya zilizokamatwa na Mamlaka, pamoja na kugawiwa machapisho mbalimbali yanayotoa elimu kwa kina zaidi.

Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Elimu Jamii Adrick Ndwelwa amesema kuwa lengo kuu la ushiriki wa Mamlaka katika Wiki ya Vijana ni kuhakikisha elimu ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya inawafikia vijana kwa njia sahihi, ili wawe mabalozi wazuri wa mapambano haya katika jamii zao.

“Vijana ndio nguvu kazi ya taifa, na ndio kundi lililo hatarini zaidi kuathiriwa na matumizi ya dawa za kulevya. Tunatumia fursa hii kuwapa elimu sahihi ili wajue madhara yake na kuepuka kujiingiza katika matumizi au biashara haramu,” alisisitiza Ndelwa.

Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2025 yamejumuisha pia maonesho ya bidhaa za wajasiriamali, ubunifu wa teknolojia na huduma mbalimbali.