Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

Askari Wanafunzi wa TFS Waelimishwa Kuhusu Dawa za Kulevya

Imewekwa: 13 October, 2025
Askari Wanafunzi wa TFS Waelimishwa Kuhusu Dawa za Kulevya

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imetoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya kwa zaidi ya askari wanafunzi 360 wa Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS) katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha TFS kilichopo Mlele, mkoani Katavi. Mafunzo hayo yametolewa kwa lengo la kuwaongezea uelewa askari hao juu ya tatizo la dawa za kulevya na mchango wao katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa hizo nchini.

Pamoja na elimu hiyo, DCEA pia ilitoa mada maalum kuhusu uhusiano uliopo kati ya uhalifu wa dawa za kulevya na uharibifu wa misitu, ikieleza namna ambavyo wazalishaji wa dawa za kulevya hukata miti katika maeneo ya misitu kwa lengo la kufanikisha kilimo cha bangi na mirungi.

Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo, Nolan Noel askari mwanafunzi amesema mafunzo hayo yamemsaidia kujua aina mbalimbali za dawa za kulevya na athari zake kwa jamii. 

“Elimu hii imenipa mwanga wa kutengeneza ushirikiano  bora baina ya mimi askari wa wakala wa huduma ya misitu Tanzania na askari kutoka DCEA ili kuweza kushirikiana katika udhibiti. Mbali na kuathiri vijana wa Kitanzania, kilimo cha dawa za kulevya pia huathiri misitu yetu ambayo sisi tunajukumu la kuilinda kwa ajili ya vizazi vijavyo” Amesema Noel

Nae mwezeshaji kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Said Madadi amesema lengo la mafunzo hayo ni kutekeleza mkakati wa kupunguza uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya hususani dawa za mashambani (bangi na mirungi) na kuimarisha mahusianao kati ya DCEA na TFS hususani kwenye mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya.

“Dawa hizo zinazalishwa kwenye misitu. Hivyo tuko hapa kuwaelimisha ili waweze kuzuia uzalishaji wa dawa za kulevya za mashambani kwenye maeneo yao. Biashara ya dawa za kulevya ni uhalifu wa kupangwa ambao unavuka mipaka hivyo kwa kushirikiana na wakala wa ihifadhi wa misitu pamoja na Taasisi au vyombo vingine itasaidia kuondoa au kupubguza kwa kiasi kikubwa tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini” amesisitiza Madadi

Kwa upande wake Emmanuel Mwaitare ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na  DCEA katika kupambana na kilimo cha dawa za kulevya na kuhakikisha misitu inabaki salama. Pia amewaomba wanafunzi askari wasitumie dawa za kulevya wala kula njama za kusaidia uzalishaji wa dawa hizo.

TFS ina nafasi kubwa katika mapambano haya kwani inahusika moja kwa moja na uhifadhi wa misitu na mazao yake, hivyo inanafasi ya kuhakikisha maeneo ya hifadhi hayageuki mashamba ya dawa za kulevya.