Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Kilo 16.643 za Dawa za Kulevya Zakamatwa jijini Dar es Salaam

Imewekwa: 07 December, 2022
Kilo 16.643 za Dawa za Kulevya Zakamatwa jijini Dar es Salaam

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata kilo 16.643 za dawa ya kulevya jijini Dar es Salaam.

Kati ya dawa hizo,kilo 15.19 ni heroin, gramu 655.73 za cocaine na gramu 968.67 ni dawa za kulevya aina ya Methamphetamine zilizowahusisha jumla ya watuhumiwa saba.

Hayo yamebainishwa leo Disemba 7, 2022 na kamishna jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Musabila Kusaya wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Kamishna Kusaya amesema kuwa, Ukamataji wa kilo 15.19 za dawa za kulevya aina ya heroin zilizowahusisha watuhumiwa watatu ni mwendelezo wa operesheni zilizopita. “Watuhumiwa hawa ni washirika wa Kambi Zuberi Seif na wenzake waliokamatwa wakiwa na kilo 34.89 za heroin katika operesheni ya mwanzoni mwa mwezi Novemba 2022,” amesema Jenerali Kusaya.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Suleman Thabit Ngulangwa mwenye umri wa miaka 36 ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Salasala, Sharifa Seleman Bakar mwenye umri wa miaka 41 ambaye ni mkazi wa Maji matitu - Mbagala na Farid Khamis Said umri miaka 22 na mkazi wa Maji matatu, Mbagala na wote ni wakazi wa Dar es Salaam.


gt


Wakati huo huo, Kamishna Jenerali Kusaya amewataja watuhumiwa wengine wanne waliokamatwa na gramu 655.75 za cocaine na gramu 968.67 za Methamphetamine wakiwa kwenye harakati za kusafirisha dawa hizo za kulevya kwenda nje ya nchi.

Watuhumiwa hao wanne ni Hussein Rajab Mtitu mwenye umri wa miaka 28 anayejulikana pia kama Chodri Mohamed ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Kibonde maji, Mbagala. Mwingine ni Jaalina Rajab Chuma mwenye umri wa miaka 31 anayejulikana pia kama Jaalina Mohan ambaye ni mjasiriamali na mkazi wa Tandika, mwingine ni Shabani Abdallah Said mwenye umri wa miaka 36 na mkazi wa Kilimahewa, Tandika, hawa pia ni wakazi wa Dar es Salaam.

“Mtuhumiwa mwingine ni Irene Dickson Mseluka mwenye umri wa miaka 39ambaye yeye ni mfanyabiashara na mkazi wa Ndala Shinyanga. Watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani mara baada ya taratibu za kiupelelezi kukamilika” amesema Jenerali Kusaya.

Pamoja na hayo, kamishna jenerali Kusaya ametunia nafasi hiyo kuwaonya wasanii wanaotumia na wanaohamasisha matumizi ya dawa za kulevya kupitia kazi zao za sanaa akiahidi kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“kuna wasanii wanahamasisha matumizi ya dawa za kulevya. Wengine wanahamasisha matumizi ya bangi lakini hili tutalifanyia kazi. Kama kuna wasanii wanaotunga nyimbo ambazio sio za kuelimisha jamii badala yake wanatunga nyimbo za kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya tutawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria” amesema Jenerali Kusaya.

Aidha, amewaomba waandishi kutumia taaluma yao kuwaeleza watanzania madhara ya dawa za kulevya.


Mwisho