Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Kigogo wa Dawa za Kulevya Raia wa Nigeria na Watanzania Wawili Wakamatwa na Zaidi ya Kilo 270 za Heroin!

Imewekwa: 16 April, 2020
Kigogo wa Dawa za Kulevya Raia wa Nigeria na Watanzania Wawili Wakamatwa na Zaidi ya Kilo 270 za Heroin!

Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya jana tarehe 15 April 2020, imefanikiwa kumkamata kigogo wa dawa za kulevya raia wa Nigeria Kanayo David Chukwu (39) mkazi wa Masaki na raia wawili wa Tanzania Alistair Amon Mbele (38) ambaye ni mkutubi wa chuo kikuu cha Aghakan jijini Dar es Salaam, mkazi wa Mbezi Kibanda cha mkaa na Isso Romward Lupembe (49) mkazi wa Mbezi Louis na Changanyikeni jijini Dar es Salaam.

Watuhumiwa wamekamatwa na dawa za kulevya aina ya heroin zinazokadiliwa kuwa na zaidi ya kilogramu 270 zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye moja ya nyumba iliyopo Mbezi kibanda cha mkaa.

J

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka James W. Kaji amesema watuhumiwa hao wamekuwa wakifanya biashara hiyo kwa muda mrefu nchini. Mamlaka imefanikiwa kuwakamata kutokana na jitihada na ushirikiano uliopo kati ya nchi yetu na nchi nyingine katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya dunia kwa kubadirishana taarifa ambazo zilipelekea kurahisisha ukamataji huo. “Baada ya kupata taarifa kutoka kwa vyombo mbalimbali vya usalama ndani na nje ya nchi tulianza kuwafuatilia toka tarehe nane na kufanikiwa kuwaweka mtegoni tangu wakiwa wanateremsha mzigo na kufanikiwa kuwakamata. amesema kamishna Kaji”

Pia watuhumiwa hao walikuwa wamefanya maandalizi ya kupokea mzigo huo kwa kujenga chemba juu ya tenki la maji machafu kwaajili ya kuhifadhia dawa hizo, na bahati mbaya mzigo uliwahi kufika kabla chemba haijakamilika hivyo kulazimika kuzihifadhi ndani ya nyumba.

J

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imewataka wananchi kuunga mkono jitihada za serikali katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya kwaajili ya kuokoa maisha ya watanzania kwa kutoa taarifa pale wanapoona matukio yasiyo ya kawaida kwa usalama. “Kilo hizi ni nyingi sana zingeingia mtaani zingeathiri nguvu kazi ya vijana wetu huko mitaani kwa kiasi kikubwa. Ninasikitika kuona bado kuna watu wasio na utu wanaendelea kujitafutia kipato kwa njia hii haramu bila kujali. Ninatoa rai kwa watanzania walio tayari kuwapambania watoto wao kuendelea kushirikiana na Mamlaka kuwafichua watu hawa bila woga” amesema kamishna Kaji.

Watuhumiwa wako mikononi mwa Mamlaka na watafikishwa mahakamani mara baada ya taratibu za upelelezi kukamilika.