MKUU WA WILAYA TEMEKE ATOA WITO KWA JAMII KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda, ametoa wito kwa jamii kushirikiana na Serikali katika kuzuia matumizi na biashara ya dawa za kulevya, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha kinga na kukata mnyororo wa usambazaji na matumizi ya dawa hizo ili kulinda afya na mustakabali wa wananchi, hususan vijana.
Mhe. Mapunda ametoa wito huo wakati akizungumza katika Tamasha la Kupiga Vita Dawa za Kulevya lililoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na kufanyika tarehe 23 Julai, 2026 katika Viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke, Dar es Salaam
Amesema changamoto ya dawa za kulevya inahitaji ushiriki wa kila mmoja kwa kuwa madhara yake hayaishii kwa mtumiaji pekee, bali huathiri familia, jamii na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Akielezea ukubwa wa changamoto hiyo katika Wilaya ya Temeke, Mhe. Mapunda amebainisha kuwa Kituo cha Methadone cha Temeke kimesajili zaidi ya watu 2,500 wanaopatiwa matibabu ya uraibu wa heroini kupitia tiba ya methadone. Aidha, amesema tangu mwaka 2022 zaidi ya watu 14,000 wamehudumiwa katika Kitengo cha Afya ya Akili cha Temeke kutokana na matatizo yanayohusishwa na matumizi ya dawa za kulevya.
Amesema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuongeza nguvu katika hatua za kinga, utoaji wa elimu na ushirikishwaji wa jamii ili kuzuia watu zaidi, hususan vijana, kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya.
Mhe. Mapunda amesema mazingira na jiografia ya Temeke yanaifanya Wilaya hiyo kuwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji uangalizi na ushirikiano mkubwa wa jamii katika kuzuia usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya.
Amesisitiza kuwa mapambano hayo yanapaswa kulenga pande zote mbili za tatizo kwa kukata mnyororo wa usambazaji wa dawa za kulevya na wakati huohuo kupunguza mahitaji yake katika jamii.
“Tusipokuwa na watumiaji, mzigo hautafika mtaani kwa sababu hautakuwa na soko. Ndiyo maana tunapaswa kupambana na usambazaji lakini pia kuhakikisha tunazuia watu kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya,” amesema Mhe. Mapunda.
Kwa upande wake Dkt. Cassian Nyandindi, akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema mapambano dhidi ya dawa za kulevya hayawezi kufanikiwa kwa juhudi za Serikali pekee, bali yanahitaji ushiriki wa wananchi, familia, taasisi na wadau mbalimbali.
Dk. Nyandindi amesema DCEA inatekeleza majukumu yake kupitia maeneo makuu manne ambayo ni kudhibiti biashara na usambazaji wa dawa za kulevya na kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria; kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya dawa hizo; kuimarisha huduma za tiba na utengemao kwa watu wenye matatizo ya uraibu; pamoja na kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kuanzia ngazi ya jamii hadi kimataifa.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kuanza kuwapa watoto elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya wakiwa katika umri mdogo, akisisitiza kuwa kinga ni nyenzo muhimu katika kuwalinda watoto na vijana dhidi ya kuingia katika matumizi na biashara ya dawa hizo.
Tamasha hilo liliwakutanisha wananchi na wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya na kujumuisha matembezi, elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya, michezo na burudani pamoja na huduma za ushauri na uhamasishaji kuhusu tiba na utengemao.