Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA na TAKUKURU Kushirikiana

Imewekwa: 19 April, 2023
DCEA na TAKUKURU Kushirikiana

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wamekubaliana kushirikiana katika kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya na kupiga vita vitendo vya rushwa Nchini.

Taasisi hizo zimefikia maamuzi hayo baada ya kubaini kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya kwa kiasi kikubwa hutumia rushwa kufanikisha usafirishaji wa dawa za kulevya kwa kuwashawishi watu wasio waaminifu ili wawasaidie kukamilisha uharifu huo katika maeneo mbalimbali nje na ndani ya nchi.

Ushirikiano baina ya DCEA na TAKUKURU utajikita zaidi katika utoaji wa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya na kupiga vita rushwa kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuoni kupitia vilabu vya kupiga vita rushwa mbazo sasa zitatumika kupiga vita rushwa na dawa za kulevya.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo amesema, Mamlaka ya Kuidhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imeona ni vema ikashirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kupanua wigo wa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya.

"Ushirikiano huo ni muhimu kwani utaisaidia sehemu kubwa ya jamii hasa wanafunzi ambao baadhi yao kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya wakiwa katika umri mdogo, kufahamu madhara ya dawa za kulevya na hatimaye kutoshiriki kwenye matumizi na biasha ya dawa hizo' amesema kamishna jenerali Lyimo..

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa CP. Salum Rashid Hamduni, amebainisha kuwa, anatambua ushirikiano baina ya Taasisi hizi utaleta tija katika mapambano dhidi ya Rushwa na tatozo la dawa za kulevya nchini hivyo ni muhimu taasisi hizo zikajipanga kikamilifu katika kuhakikisha kuwa jukumu hilo linatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.

Aidha, amesema kuwa, ushirikino huo usijikite tu katika utoaji wa elimu juu ya Rushwa na Dawa za kulevya bali pia katika kubadilishana uzoefu wa namna ya kukabiliana makosa ya rushwa, kwani ni wazi kuwa, idadi kubwa ya watu wanaokutwa na makosa hayo pia hukutwa na makosa ya rushwa na uhujumu uchumi.

Makubaliano hayo yamefanyika jijini Dodoma, katika Ofisi za Makao Makuu ya TAKUKURU yaliyohudhuriwa pia na baadhi ya Maafisa kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.


f

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa CP. Salum Rashid Hamduni (kulia) akisisitiza jambo wakati wa kikao na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya - DCEA (kushoto).


f

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa CP. Salum Rashid Hamduni (kulia) akimkabidhi zawadi Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za KUlevya Aretas Lyimo (kushoto) walipotembelea ofisi za TAKUKURU Dodoma.


f

Kamishna wa Kinga na Tiba kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Dkt. Perter Patrick Mfisi (aliye nyoosha mkono) akiwasilisha jambo katika kikao hicho.