Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )
Dawa za Kulevya zilivyokula Nusu ya Maisha Yangu
Dawa za Kulevya zilivyokula Nusu ya Maisha Yangu

Naitwa Saidi Bandawe, nina umri wa miaka 43, ni mkazi wa Tanga. Nilianza matumizi ya dawa za kulevya nikiwa mdogo sana.Nilianza na petroli, nikaja bangi, pombe, nikaeendelea kwenye Heroin cocaine na aina zote za vilevi. Lakini sikuwa na taarifa na tatizo langu.

Nimetumia mihadarati kwa zaidi ya miaka 22. Kwahiyo kimahesabu mimi ni kama kijana wa miaka 22 maana miaka mingine yote imeliwa na matumizi ya dawa za ulevya. Kitu kilichonifanya mimi niachane na matumizi ya mihadarati ni kwamba; Baada ya ndugu yangu kuolewa mimi nilikwenda kwake nikamkaba na kumpora pete yake ya ndoa, kisha nikatorokea Zanzibar. Kitendo kile kilimkera ndugu yangu sana na kunitamkia kwamba yeye sio ndugu yangu tena. nikiwa Zanzibar nilipata taarifa kwamba ndugu yangu yule amefariki, hivyo kunilazimu kutoka Zanzibar kuja Tanga kwenye msiba. Kitendo cha mimi kutoka Zanzibar mpaka tanga nikakuta ndugu yangu ameshazikwa.

Kile kitendo kiliniuma sana kwa sababu alifariki tukiwa hatuelewani, nimemdhuru na ameniambia mimi sio ndugu yake. Ile hali ilinifanya nitafute usaidizi. Nilienda Pederef Dar es Salaam Sober House kwa miezi sita na kwa bahati mbaya nikarudia tena dawa za kulevya. Niliporejea Tanga nikasaidiwa na kituo cha Tanga drugs free kwa mwezi mmoja . sasa hivi nina miaka mitano ya usafi bila kutumia Dawa za Kulevya. Namshukuru Mwenyezi Mungu nimebadirisha mfumo wa maisha yangu. Sasa hivi nimefungua taasisi kwa kushirikiana na wenzangu kama mimi tuliokuwa katika nyumba za upataji nafuu na tunafanya programu za kuwasaidia wenzetu waachane na matumizi ya dawa za kulevya. Lakini pia nawashukuru viongozi wa Tanga akiwepo mama waziri Ummy na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya maana ndio watu walioniongoza kuachana na dawa hizi.