Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )
Mwaka mmoja bila Dawa za Kulevya
Mwaka mmoja bila Dawa za Kulevya

Kwa jina naitwa Christina, ni mwenyeji wa Iringa na ni mama mwenye watoto za wawili. Nilianza kutumia Dawa za Kulevya tarehe 24 mwezi wa 12 mwaka 2004 ambapo ilikuwa ni siku yangu ya kuzaliwa. Nilikuwa na mpenzi wangu ambae alikuwa akitumia Dawa za Kulevya. Katika siku yangu hiyo ya kuzaliwa mpenzi wangu alinishauri nivute mivuto miwili kama ishara ya kusherehekea na mimi nikachukua na kuvuta bila woga.

Changamoto nilizopitia katika utumiaji wa Dawa za Kulevya ni nyingi sana. Kwanza kabisa yule mpenzi wangu alikamatwa na kete mbili za Dawa akahukumiwa kifungo cha miaka tisa jela. Wakati huo tayari mimi alikuwa ameniacha katika utumiaji wa Dawa za Kulevya. Sikuwa na pesa ya kununulia Dawa hizo ili nitumie. Niliteseka kwa maumivu makali sana na kutokana na maumivu niliyoyapata kutokana na kukosa Dawa, nilianza kuuza vitu vyangu vya thamani mpaka ikafikia wakati nikaanza kuuza mwili wangu ili nipate pesa nikanunue Dawa za Kulevya. Niliendelea na biashara ya kujiuza na mwisho wa siku nikawa sina soko tena la kuweza kujiuza. Nilikonda na kuwa mchafu sana.

Nikajiingiza kwenye kikundi cha watoto wa mtaani. Nikaanza kuiba na kukaba watu. Nikawa najitafutia pesa kwa njia ya utapeli ili nikatumie Dawa za Kulevya. Kadri siku zilivyozidi nilitafuta kutafuta maarifa mengi na mbinu mbalimbali ili kujipatia pesa kidanganyifu.

Nikaanza kwenda duka la dawa baridi na kununua dawa ya vidonda inayoitwa Iodine na plasta.Nikawa napakaa ile dawa kwenye tumbo la uzazi naweka na yake maplasta. Nikishafunga, ile dawa inaonekana kama damu kisha naingia mtaani kuomba omba nikijidai niefanyiwa upasuaji na nimetoka hospitali kwahiyo nahitaji pesa za kukidhi mahitaji ya matibabu kumbe ilikuwa uongo.

Nimeteseka kwa miaka sana ila namshukuru Mungu leo hii nimetimiza mwaka mmoja wa kutotumia Dawa yoyote ya Kulevya. Nawashukuru wale wote walionisaidia na kunipambania katika upataji nafuu wangu. Namshukuru sana baba yangu Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa kutupatia viongozi wanaoibeba shida ya mtu na kuifanya kama yao, pia namshukuru baba yangu Mhe. Kassim Majaliwa aliniona pale Iringa mwaka jana katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kupiga vita Dawa za Kulevya na amenisaidia sana. Tatu ni kwa mama yangu Mhe. Jenista Mhagama popote alipo Mungu ambariki, nne ni kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wamekuwa msaada mkubwa kwangu wameweza kunisimamia katika kipindi hiki chote mpaka leo nimekuwa binadamu kamili na kuweza kusimama hapa mbele yenu kutoa ushuhuda.

j