Elimu ya Dawa za Kulevya Yaendelea Kuwafikia Maelfu Kanda Mbalimbali
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeendelea kutekeleza mkakati wake wa kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya kupitia kampeni za elimu kinga kwa makundi mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya mpango endelevu wa kuisaidia jamii kutambua, kuepuka na kupambana na matumizi pamoja na biashara ya dawa hizo. Katika wiki ya pili ya Novemba 2025, shughuli mbalimbali za uelimishaji zimefanyika kupitia redio, makongamano na matukio ya kijamii na kuwafikia wanafunzi, wanamichezo, wazazi na umma kwa ujumla
KANDA YA PWANI
DCEA kanda ya Pwani ilitoa elimu kwa wanachuo wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) katika kampasi za Mtwara na Lindi ikiwa ni sehemu ya programu ya orientation ya mwaka wa masomo 2025/2026. Wanafunzi wapya na wanaoendelea walipatiwa elimu kuhusu sababu za matumizi ya dawa za kulevya, namna ya kujiepusha, madhara ya kiafya, aina za dawa zinazopatikana zaidi nchini, na huduma kwa waraibu. Aidha, Kanda ya Pwani iliendelea na kampeni yake kupitia michezo, ambapo zaidi ya wanamichezo 700 kutoka timu ya Veterani na washiriki wa tamasha la kuitambulisha timu ya Rahaleo Sports Club mjini Lindi walipatiwa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya kwa ujumla na kusisitizwa kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kwa kupinga matumizi ya dawa za kulevya ili kulinda afya na uwezo wao michezoni.


KANDA YA KASKAZINI
Waelimishaji kutoka Kanda ya Kaskazini walitoa elimu kupitia vituo vya redio vya TBC Arusha, Sunrise FM, Revival FM na One Radio za mkoani Arusha. Elimu hiyo iliangazia madhara ya dawa za kulevya, namna zinavyoathiri mfumo wa fahamu, na dalili za awali za matumizi ambazo wazazi wanaweza kuziona kwa watoto wao.Maandalizi kuelekea kufunguliwa kwa vyuo yamefanya elimu hii kuwa ya muhimu zaidi, ambapo wanafunzi walipewa angalizo kuhusu vishawishi vinavyoweza kuwakabili na namna matumizi ya dawa za kulevya yanavyoweza kuharibu ndoto zao za kitaaluma kabla hazijaanza kutimia.
Pamoja na uelimishaji huo, DCEA kanda ya kaskazini ilishiriki Kongamano la 16 la Afya ya Akili lililofanyika KCMC Moshi tarehe 7–8 Novemba 2025, ambapo afisa elimu jamii Bw. Shabani Miraji, aliwasilisha mada kuhusu uhusiano wa uraibu wa dawa za kulevya na magonjwa ya akili na kusisitiza namna matumizi ya bangi yanavyoweza kuchochea au kuamsha matatizo ya afya ya akili. Vilevile, wanafunzi 120 wa VETA Manyara na VETA Gorowa (Babati) walipatiwa mafunzo kuhusu mbinu mpya za ushawishi, madhara ya dawa za kulevya, na namna ya kuwa mabalozi wa kutoa elimu sahihi katika jamii.



KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI
Katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, wanafunzi 203 wa Open University Kampasi ya Mbeya walipatiwa elimu kinga dhidi ya dawa za kulevya. Maofisa wa DCEA walibainisha mabadiliko ya mbinu za usambazaji, ikiwemo ujio wa bidhaa zenye mbegu au viambato vya dawa za kulevya vilivyofichwa kwenye vyakula kama biskuti na pipi vinavyolengwa kwa vijana. Wanafunzi walihimizwa kuwa makini na kuimarisha uwezo wao wa kutambua mazingira hatarishi, huku wakitengenezwa kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii.
KANDA YA KATI
Kupitia Dodoma FM, elimu ya dawa za kulevya ilitolewa kwa umma na iliwalenga ikiwaelekeza wanafunzi wapya wa vyuo vikuu na vya kati wanaotarajia kuanza masomo kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya wakati wa maisha ya chuo. Pia, elimu hiyo imetolewa kwa wanafunzi zaidi ya 1800, walimu pamoja na wazazi walioshiriki kwenye siku ya utamaduni wa mtanzania katika shule ya East Africa jijini Dodoma.


Elimu kwa jamii kwa Mwezi Novemba, kwa kiasi kikubwa imelenga kuwasaidia wanachuo kujiepusha na uraibu, kulinda ndoto zao za kitaaluma, na kuimarisha ushirikiano wa jamii katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo ilieleza kuwa baadhi ya wanachuo tayari wamekwishakamatwa wakiwa na dawa za kulevya, jambo linaloonyesha hatari zinazowakabili vijana wa umri wa chuo.
MWISHO