Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Siku 365 za Rais Samia Katika Kupambana na Dawa za Kulevya

Imewekwa: 11 March, 2022
Siku 365 za Rais Samia Katika Kupambana na Dawa za Kulevya

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Musabila Kusaya ametoa taarifa ya mafanikio ya mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan katika mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa wanahabari Machi 10, 2022, amesema Mamlaka imedhibiti uingizwaji wa tani 120.5 za kemikali bashirifu (yabisi), pamoja na lita 40 za kemikali hiyo (kimiminika) ambazo zilikuwa zikiingizwa Nchini. Kufuatia udhibiti huo Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) limeitambua Tanzania kama kinara wa udhibiti wa kemikali hizo katika nchi za afrika mashariki na hivyo kuiteua kutoa mafunzo kwa nchi nyingine tisa (9) ambazo ni Rwanda, Burundi, Madagascar, Zambia, Malawi, Ethiopia, Msumbiji, Eritrea na Mauritius.

katika kipindi hicho pia, Mamlaka ilifanikiwa kukamata watuhumiwa 11,712 wa dawa za kulevya, ambao walikutwa na kilo 35, 227. 25 za dawa aina mbalimbali, hekari 185 za mashamba ya bangi na hekari 10 za Mirungi.

Pia, jumla ya watuhumiwa 100 walikutwa na dawa aina ya Cocaine, watuhumiwa 588 walikamatwa wakiwa wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya Heroin, watuhumiwa 9,484 walikamatwa wakijihusisha na dawa za kulevya aina ya bangi, watuhumiwa 1,395 walikamatwa na mirungi. Vilevile watuhumiwa walikamatwa kwa kumiliki mashamba ya bangi na watuhumiwa wawili walikutwa na mashamba ya mirungi.

Mamlaka imeimarisha ushirikiano na Taasisi za Serikali na za Kimataifa katika kudhibiti uchepushwaji wa Kemikali Bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya. Taasisi hizo ni pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Baraza la Famasi (PC) pamoja na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (INCB). Aidha, Mamlaka kwa kushirikiana na Taasisi za udhibiti za Serikali imeanzisha Mradi wa ushirikiano kati ya Serikali na Taasisi binafsi katika kudhibiti uchepushwaji wa kemikali bashirifu ambapo Kampuni 27 za kemikali bashirifu na vyama viwili (2) vya wadau wanaohusika na dawa za binadamu vimetia saini mkataba wa makubaliano wa kuanzishwa kwa ushirikiano huo.

Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Taasisi zingine zisizo za Kiserikali imefanikiwa kupanua huduma za tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya nchini. Katika mwaka 2021, Kliniki sita (6) kwa ajili ya tiba ya Methadone (MAT Kliniki) zimefunguliwa. Kliniki moja (1) mkoani Songwe katika mji wa Tunduma, Kliniki moja (1) Jijini Arusha na Kliniki zingine nne (4) Jijini Dar es Salaam katika maeneo ya Tegeta, Segerea, Mbagala na Kigamboni na hivyo kufanya jumla ya Kliniki kumi na tano (15) nchini, zikihudumia zaidi ya waathirika 10,600 kila siku. Vilevile, Mamlaka imekuwa ikisimamia upatikanaji wa uhakika wa dawa ya Methadone kwa ajili ya tiba ya waraibu wa Heroin kwa kusimamia uagizaji, usambazaji na udhibiti wake.

Katika kuwasaidia waraibu waliopata nafuu, Mamlaka kwa kushirikiana na Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi iliyopo Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa programu ya kukuza Ujuzi kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya. Vijana wapatao 200 wanaopatiwa matibabu kwenye Kliniki za Methadone watapatiwa nafasi katika vyuo vya VETA, SIDO na vinginevyo kulingana na mahitaji yao ya fani walizonazo. Aidha, wahitimu wa programu hii watapewa vifaa vya kazi kwa ajili ya kuwawezesha kufanya shughuli za kujiingizia vipato. Programu hii ni endelevu na itakuwa ikichukuwa waathirika waliopata nafuu na kukuza ujuzi wao katika fani mbalimbali.

Ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, Mamlaka iliratibu na kusimamia uendeshwaji wa nyumba 45 za upataji nafuu (Sober houses) katika mikoa ya Kilimanjaro,Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Dodoma, Morogoro, Iringa, Mwanza, Kagera, Tabora na Arusha.

Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto na wadau wengine imeandaa mwongozo utakaotumika kutoa huduma ngazi ya jamii kwa waraibu wa dawa za kulevya Nchini. Pia, Mamlaka imefanikiwa kuandaa mwongozo wa uelimishaji juu ya tatizo la dawa za Kulevya Nchini ambao utatumiwa na wadau mbalimbali kutoa elimu katika makundi mbalimbali ya kijamii.

Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu imeweza kuanzisha vilabu vya kupinga dawa za kulevya mashuleni na kutoa elimu kwa walimu 66 ili kuwawezesha kusimamia klabu hizo shuleni. Aidha, Elimu juu ya tatizo la matumizi na biashara ya dawa za kulevya iliwafikia wanachuo 1,700 katika vyuo mbalimbali nchini. Vilevile, elimu bora kuhusu tatizo la dawa za kulevya imekuwa ikitolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari, warsha, makongamano na maadhimisho mbalimbali na kufanikiwa kuwafikia takribani wananchi 28,000.

Mamlaka imezijengea uwezo Asasi za Kiraia 77 katika mwaka 2021 ambazo zinatoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya kwa jamii katika mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Pwani, Tanga, Arusha, Mbeya, Songwe, Morogoro, Ruvuma,Tabora, Shinyanga, Njombe, Iringa, Lindi, Simiyu na Mtwara. Asasi hizi zimekuwa zikitoa mchango mkubwa katika kuelimisha jamii.

Mafanikio haya yamewezekana kutokana na utashi wa kisiasa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, ambapo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa mstari wa mbele kuviwezesha vyombo vinavyojihusisha na udhibiti wa dawa hizo Nchini.