Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Serikali Yawakumbuka Waathirika wa Dawa za Kulevya - Tanga

Imewekwa: 02 July, 2020
Serikali Yawakumbuka Waathirika wa Dawa za Kulevya - Tanga

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezindua kituo cha muda cha kutoa huduma ya Methadone kwa waraibu wa dawa za kulevya aina ya heroin. Kituo hicho kimezinduliwa tarehe 24 Juni, 2020 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu katika hospitali ya Bombo mkoani Tanga.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Ummy amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya waathirika wa dawa za kulevya kati ya 200,000 hadi 350,000 kwa mujibu wa takwimu za wizara ya afya. Kati yao waathirika takribani 30,000 wanatumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga huku kukiwa na makadirio ya asilimia 35% ya kiwango cha maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwenye jamii ya waathirika hao. Amesema kuwa kiwango hicho ni kikubwa karibu mara tano zaidi ya kiwango cha maambukizi kwenye jamii hiyo kwa mwaka 2014.y

Sambamba na hayo, hali ya maambukizi mapya katika kundi hilo kwa sasa yamepungua hadi kufikia mdungaji mmoja katika kila wanaojidunga 10 ikilinganishwa na wanaojidunga 4 kati ya 10 kwa mwaka 2014. “Utafiti iliyofanyika mwaka 2016 unaonyesha kuwa Mkoa wa Tanga una zaidi ya waathirika 5,190 na hivyo kuufanya mkoa huo kuwa wa pili nchini kwa kiwango cha maambukizi” amesema Waziri Ummy.

“Mkoa wa Tanga unaidadi kubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya hali inayosababisha ongezeko la watumiaji kutokana na uwepo wa mazingira chochezi ya utumiaji tofauti na mikoa mingine hapa nchini,” amesema Mhe. Ummy.

Ameongeza kuwa kutokana na changamoto hiyo, serikali iliamua kuja na tiba ya bure ya dawa ya methadone kwa ajili ya kuwahakikishia tiba waathirika wa dawa za kulevya.

“Lengo la serikali ni kufungua vituo sita katika maeneo yenye viwango vikubwa vya maambukizi, ili kufika mwisho wa mwaka 2020 serikali itakuwa imesogeza huduma hiyo karibu na wananchi” amebainisha Waziri Ummy.

Naye Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, James Wilbert Kaji amesema kuwa uwepo wa kituo hicho ni mpango wa kufikisha huduma kwa walengwa kwa haraka, na ufunguzi wa kituo hicho ni muendelezo wa uwepo wa vituo nane ambavyo tayari vinatoa huduma ya methadone kwa waraibu wapatao 8,500 kila siku.

J

Hata hivyo Kaji ameishukuru serikali kwa kuja na mtaala wa athari za dawa za kulevya ambao utaanza kutumika mashuleni kuanzia darasa la tatu hadi sekondari ambao utasaidia kutoa elimu ya janga hilo.

Mkurugenzi wa Shirika la Amref Dkt Florence Temu amesema kuwa Shirika hilo limeamua kuunga mkono jitihada za serikali kupambana na ugonjwa huo kwa kuanzia na uanzishwaji wa kituo cha muda ambacho kimegharimu kiasi cha shilingi milioni 14.

Amesema “uwepo wa huduma hiyo utasaidia jamii ya Wanatanga wanaohitaji huduma hiyo kwa kiasi kikubwa.”

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Jonathan Budemu amesema hadi kukamilika jengo hilo, serikali inatarajia kutumia kiasi cha shilingi milioni 786. Amewaomba wananchi pamoja na wadau wengine kuwashawishi waathirika wa dawa za kulevya kufika katika kituo hicho kwa ajili ya kupata huduma za tiba na ushauri