Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA Yaweka Rekodi, Kilogramu 2,327,983.66 za Dawa za Kulevya Zakamatwa 2024

Imewekwa: 09 January, 2025
DCEA Yaweka Rekodi, Kilogramu 2,327,983.66 za Dawa za Kulevya Zakamatwa 2024

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha taifa linakombolewa kutoka katika janga hili linalohatarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, amesema mafanikio makubwa yamepatikana mwaka 2024 kwa kukamatwa kwa kiasi kikubwa cha dawa za kulevya na kuimarika kwa juhudi za kutoa elimu, tiba kwa waraibu, na ushirikiano wa kimataifa.

“Jumla ya kilogramu 2,327,983.66 za dawa za kulevya zilikamatwa mwaka huu, idadi ambayo haijawahi kufikiwa tangu kuanza kwa mapambano haya nchini. Dawa zilizokamatwa zilijumuisha bangi aina ya skanka na hashishi, methamphetamine, heroin, na dawa tiba zenye asili ya kulevya kama fentanyl. Aidha, kwa mara ya kwanza, dawa mpya aina ya 3-4 Methylene-Dioxy-Pyrovalerone (MDVP) ilikamatwa nchini” amesema Lyimo.

Aidha, ameongeza kuwa kiasi kikubwa cha dawa kilikamatwa kupitia operesheni za kimkakati zilizofanyika katika maeneo mbalimbali, yakiwemo maeneo ya Bahari ya Hindi.

“Operesheni hizi zilifanikiwa kuzuia kilogramu 673.2 za methamphetamine na heroin kuingia nchini, ambapo kilogramu 448.3 zilinaswa ndani ya jahazi lililosajiliwa nchini Pakistan likiwa na raia wanane wa Pakistani. Kilogramu nyingine 224.9 zilikamatwa kwenye fukwe za Dar es Salaam” ameongeza Lyimo.

Katika juhudi za kuzuia madhara ya dawa za kulevya, serikali ilitoa elimu kwa takribani watu milioni 28 kupitia vyombo vya habari, semina, warsha, matamasha, na matukio ya kitaifa.

Kwa upande wa tiba, vituo viwili vipya vya matibabu ya waraibu wa dawa za kulevya (MAT Clinics) vilifunguliwa katika mikoa ya Pwani na Tanga, na kufikisha jumla ya vituo 18 nchini. Vituo hivi vimeweza kuhudumia waraibu 18,170 mwaka huu. Aidha, nyumba za upataji nafuu (sober houses) ziliongezeka kutoka 56 hadi 62, zikiwahudumia waraibu 17,230.

Kamishna Lyimo alieleza kuwa serikali imeendelea kutoa msaada mkubwa kwa waraibu wa dawa za kulevya kupitia huduma za afya ya akili katika hospitali za wilaya, mikoa, na rufaa, ambapo zaidi ya waraibu laki tisa walihudumiwa.


Hata hivyo kamishna Lyimo amebainisha kuwa bado kuna changamoto ya upatikanaji wa dawa mpya za kulevya zinazotengenezwa kwa lengo la kukwepa sheria.

“Tumegundua baadhi ya watu wameanza kutengeneza dawa mbadala zinazofanana na heroin kutokana na uhaba wa dawa hiyo. Tunawafuatilia kwa karibu na tumeanza kuchukua hatua kali dhidi yao,” alisema Kamishna Lyimo.

Katika kuitatua changamoto hiyo, ameahidi kuwa kwa mwaka 2025, DCEA imelenga kutumia teknolojia za kisasa kufuatilia mitandao ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kuongeza ushirikiano wa kimataifa na elimu kwa jamii itaendelea kupewa kipaumbele ili kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na wananchi.

Kamishna Lyimo alitoa shukrani za dhati kwa vyombo vya ulinzi na usalama, wadau wa maendeleo, na waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla huku akiomba ushirikiano wa wananchi kutoa taarifa kupitia namba ya bure 119 kwani vita dhidi ya dawa za kulevya si jukumu la serikali pekee, bali ni jukumu la kila Mtanzania mwenye mapenzi mema kwa taifa la Tanzania.

MWISHO