Kilimo cha bangi Mkoa wa Mara Chapungua kwa Asilimia 80 Kufuatia operesheni Endelevu za Serikali
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, amesema kilimo cha bangi katika Mkoa wa Mara kimepungua kwa takribani asilimia 80 kufuatia operesheni endelevu zinazotekelezwa na Serikali za kudhibiti na kutokomeza uzalishaji wa dawa za kulevya nchini.
Akizungumza leo, Julai 24, 2026, baada ya kuhitimisha operesheni maalumu zilizotekelezwa katika Wilaya za Tarime na Rorya, Kamishna Jenerali Lyimo alisema operesheni hizo zimefanikisha kuteketezwa kwa mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 291.2, kukamatwa kwa magunia 15 ya bangi kavu pamoja na pikipiki nne zilizokuwa zikitumika katika shughuli hizo haramu. Aidha, watu wawili walikamatwa, huku uchunguzi ukiendelea kuwabaini na kuwakamata washirika wengine wa mtandao huo wa kihalifu.
Alisema mafanikio hayo yanadhihirisha ufanisi wa operesheni endelevu zinazotekelezwa na Serikali, akibainisha kuwa mwaka 2024 zaidi ya ekari 3,500 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika Mkoa wa Mara. Hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza uzalishaji wa bangi na kuvuruga mtandao wa kilimo hicho katika maeneo yaliyokuwa yakiathirika zaidi.
"Matokeo haya yanaonesha kuwa juhudi za Serikali zinaendelea kuzaa matunda. Wananchi wengi wameachana na kilimo cha bangi na sasa wanajihusisha na shughuli halali za uzalishaji zinazowanufaisha wao, familia zao na Taifa kwa ujumla," alisema Kamishna Jenerali Lyimo.
Kamishna Jenerali Lyimo amewataka wananchi ambao bado wanajihusisha na kilimo cha bangi kuachana na shughuli hiyo mara moja na kuelekeza nguvu zao katika kilimo halali cha mazao ya chakula na biashara pamoja na shughuli nyingine halali za kiuchumi. Aidha, aliwahimiza kuendelea kushirikiana na DCEA na vyombo vingine vya dola kwa kutoa taarifa za siri kuhusu watu wanaojihusisha na uzalishaji, usafirishaji, usambazaji na biashara ya dawa za kulevya.
Alisisitiza kuwa DCEA itaendelea kuimarisha operesheni, doria na uchunguzi wa kina katika maeneo mbalimbali nchini, pamoja na kuwachukulia hatua kali za kisheria wote watakaobainika kujihusisha na makosa ya dawa za kulevya.
Kwa upande wake, Afisa Tarafa wa Nchaje, Stephano Peter Kiabaroti, alisema uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, umeongeza uwezo wa DCEA kutekeleza operesheni zenye tija katika kudhibiti na kutokomeza kilimo cha bangi.
Alisema wananchi wengi waliokuwa wakitegemea kilimo hicho kwa sasa wamehamia katika uzalishaji halali wa mazao ya chakula na biashara pamoja na shughuli za ufugaji, hatua ambayo imeanza kuleta manufaa ya kiuchumi kwa familia zao na jamii kwa ujumla.
Naye Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Rozana, Bi. Kurwa Robert, alisema kabla ya kuimarishwa kwa operesheni hizo, kilimo, matumizi na biashara ya bangi vilichangia ongezeko la vitendo vya uhalifu katika eneo hilo, huku baadhi ya vijana wakijihusisha na makundi ya uhalifu.
Alisema tangu DCEA ilipoimarisha operesheni za kuteketeza mashamba ya bangi, hali ya usalama imeimarika kwa kiwango kikubwa na wananchi wameendelea na shughuli zao za kila siku kwa utulivu.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nkerege, Joseph Mwita Ryoba, alisema kijiji hicho kilikuwa miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi na kilimo cha bangi, ambapo mwaka 2024 zaidi ya ekari 3,000 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika operesheni za Serikali.
Alisema kwa sasa wananchi wengi wameachana na kilimo hicho na kuelekeza nguvu zao katika shughuli halali za uzalishaji, jambo linaloonesha kuongezeka kwa uelewa wa jamii kuhusu madhara ya dawa za kulevya na umuhimu wa kushiriki katika shughuli halali za maendeleo na uchumi.
_1785230490.png)
