Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA yazindua Filamu ya "Kifurushi" Kuimarisha Mapambano Dhidi ya Usafirishaji wa Dawa za Kulevya

Imewekwa: 13 July, 2026
DCEA yazindua Filamu ya "Kifurushi" Kuimarisha Mapambano Dhidi ya Usafirishaji wa Dawa za Kulevya

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imezindua rasmi filamu ya elimu Kifurushi itakayotumika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mbinu zinazotumiwa na wahalifu kusafirisha dawa za kulevya kupitia vyombo vya usafiri wa umma na kuwatahadharisha dhidi ya kubeba mizigo au vifurushi wasivyovifahamu.

Filamu hiyo imezinduliwa katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi Mwisho, jijini Dar es Salaam, na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas James Lyimo, mbele ya wawakilishi wa taasisi mbalimbali, wadau wa sekta ya usafirishaji, viongozi wa dini, wasanii, waigizaji, wananchi pamoja na waandishi wa habari.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kamishna Jenerali Lyimo alisema dawa za kulevya zinaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya za wananchi, ustawi wa familia, usalama wa jamii na maendeleo ya taifa kutokana na madhara yake ya kiafya, kijamii na kiuchumi.

"Dawa za kulevya si tatizo la mtu mmoja mmoja bali ni changamoto ya taifa zima. Athari zake zinaigusa jamii kwa ujumla na kuathiri maendeleo ya nchi katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi," alisema Lyimo.

Alisema matumizi na biashara ya dawa za kulevya huchangia kuongezeka kwa uhalifu, kuvunjika kwa familia, kudhoofika kwa nguvu kazi ya taifa na kupungua kwa tija katika shughuli za uzalishaji mali, hususan miongoni mwa vijana.

Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya kupitia operesheni za ukamataji, uchunguzi wa makosa ya dawa za kulevya, utoaji wa huduma za tiba kwa waathirika pamoja na kampeni mbalimbali za elimu kwa umma.

Kamishna Jenerali Lyimo alisema uchunguzi unaofanywa na DCEA umebaini kuwa wahalifu wanaendelea kubuni mbinu mpya za kusafirisha dawa za kulevya kupitia vyombo vya usafiri wa umma kwa kuzificha kwenye mizigo na vifurushi vinavyoonekana kuwa vya kawaida. Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi, abiria na hata wahudumu wa vyombo vya usafiri wamejikuta wakikabiliwa na mkono wa sheria baada ya kukubali kubeba mizigo wasiyoifahamu.

Alieleza kuwa hali hiyo ndiyo iliyochochea DCEA kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) pamoja na Bodi ya Filamu Tanzania (TFB) kuandaa filamu hiyo ambayo itaoneshwa katika mabasi yanayofanya safari za mikoa mbalimbali nchini ili kutoa elimu kwa wasafiri na wananchi kwa ujumla.

"Filamu hii imeandaliwa kuonesha namna ambavyo mtu anaweza kuingia katika mtego wa kusafirisha dawa za kulevya bila kujua kwa kubeba mzigo au kifurushi kisichomuhusu. Lengo letu ni kuhakikisha kila mwananchi anatambua kuwa elimu na tahadhari vinaweza kumkinga dhidi ya uhalifu huu," alisema.

Alisema filamu hiyo pia inalenga kuongeza uelewa kwa madereva, makondakta, wahudumu wa mabasi, wasafirishaji wa mizigo, abiria na wananchi kuhusu wajibu wao wa kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kutobeba mizigo wasiyoifahamu na kutoa taarifa wanapobaini viashiria vya uhalifu huo.

Aidha, Kamishna Jenerali Lyimo aliwataka wamiliki wa mabasi na makampuni ya usafirishaji kuipa kipaumbele filamu hiyo kwa kuhakikisha inaoneshwa katika vyombo vyao vya usafiri ili kila safari iwe fursa ya kutoa elimu kwa umma.

Akieleza sababu ya kuzinduliwa kwa filamu hiyo katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, alisema kituo hicho ni miongoni mwa vituo vikubwa nchini vinavyohudumia maelfu ya wasafiri kila siku, hivyo kuwa sehemu sahihi ya kuwafikia kwa wakati mmoja abiria, madereva, makondakta na wasafirishaji wa mizigo.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, alisema filamu ni nyenzo muhimu ya kufikisha elimu kwa jamii kutokana na uwezo wake wa kuwasilisha ujumbe kwa njia rahisi na inayogusa maisha ya wananchi. Alisema ushirikiano kati ya TFB na DCEA unaonesha namna tasnia ya filamu inavyoweza kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na changamoto za kijamii kupitia kazi za ubunifu.

Kadhalika,  Kamishna Jenerali Lyimo aliwataka wananchi kuwa waangalifu wanapopewa mizigo au vifurushi vya kubeba kwa niaba ya watu wengine.

"Usikubali kubeba mzigo, kifurushi au bidhaa yoyote usiyoifahamu. Hakikisha unatambua unachobeba, kinatoka kwa nani na kinaelekea kwa nani. Kifurushi unachodhani ni cha kawaida kinaweza kubeba dawa za kulevya na kubadili maisha yako kwa matokeo hasi," alisisitiza.

MWISHO