Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA Yawajengea Uwezo Waandishi wa Habari Kuhusu Hatari Mpya za Dawa za Kulevya

Imewekwa: 14 July, 2026
DCEA Yawajengea Uwezo Waandishi wa Habari Kuhusu Hatari Mpya za Dawa za Kulevya

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari katika kutoa elimu sahihi kwa umma kuhusu changamoto zinazoibuka katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Semina hiyo ililenga kuwaongezea waandishi wa habari uelewa kuhusu kemikali bashirifu (Precursor Chemicals), maabara bubu za kutengeneza dawa za kulevya (Clandestine Laboratories), dawa mpya za kulevya (New Psychoactive Substances – NPS), pamoja na matumizi mabaya ya dawa tiba zenye asili ya kulevya (Prescription Medicines).

Kwa miaka mingi, vyombo vya habari vimekuwa wadau muhimu katika kuhabarisha jamii kuhusu shughuli mbalimbali za DCEA, ikiwemo ukamataji wa dawa za kulevya, kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa, uteketezaji wa dawa za kulevya, pamoja na utoaji wa huduma za tiba na utengemao kwa waraibu wa dawa za kulevya. Hata hivyo, DCEA imebaini kuwepo kwa uhitaji wa kuongeza uelewa kuhusu mada hizo ikiwa ni maeneo yanayoendelea kujitokeza katika biashara haramu ya dawa za kulevya.

Katika semina hiyo, washiriki walipata elimu kuhusu matumizi halali ya kemikali bashirifu katika sekta mbalimbali za uzalishaji na namna kemikali hizo zinavyoweza kuchepushwa na kutumika  katika utengenezaji wa dawa za kulevya. Aidha, walielimishwa kuhusu mbinu zinazotumiwa kuanzisha na kuendesha maabara bubu za kutengeneza dawa za kulevya, aina na athari za dawa mpya za kulevya (NPS), pamoja na madhara yanayotokana na matumizi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya na dawa za kulevya kwa ujumla.

Washiriki pia walikumbushwa wajibu wa vyombo vya habari katika kuelimisha jamii kwa usahihi, kutoa taarifa zenye weledi na kusaidia wananchi kutambua vitisho vipya vinavyojitokeza katika matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa DCEA, Bi. Florence Khambi alisema kuwa, vyombo vya habari ni wadau muhimu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, hivyo kuwajengea uwezo waandishi wa habari ni mkakati unaolenga kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, zenye weledi na zinazochochea ushiriki wa jamii katika kudhibiti tatizo hilo.

Aliongeza kuwa upatikanaji wa taarifa sahihi kupitia vyombo vya habari utachangia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mbinu mpya zinazotumiwa na wahalifu wa dawa za kulevya na kuunga mkono jitihada za DCEA katika kufikia dira ya kuwa na jamii isiyotumia dawa za kulevya. Semina hiyo inatarajiwa kuongeza uwezo wa waandishi wa habari kuripoti kwa usahihi na kwa kina masuala yanayohusu kemikali bashirifu, maabara bubu, dawa mpya za kulevya na matumizi mabaya ya dawa tiba zenye asili ya kulevya, hatua itakayosaidia kuongeza uelewa wa umma na kuimarisha juhudi za taifa za kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.

DCEA itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata taarifa sahihi na elimu stahiki kuhusu mwenendo wa tatizo la dawa za kulevya, athari zake na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kulidhibiti.