DCEA na VETA Zasaini Makubaliano ya Kuwezesha Waraibu Waliopata Nafuu Kupata Ujuzi wa Ufundi Stadi
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Tanzania (VETA) zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) yenye lengo la kuwawezesha waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu kujifunza ujuzi mbalimbali wa kazi ili waweze kujitegemea na kurejea katika maisha ya kawaida.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo iliyofanyika tarehe 4 Juni, 2026 jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas James Lyimo alisema, ushirikiano huo ni sehemu ya utekelezaji wa jitihada za Serikali katika kuimarisha huduma za tiba na urejeshaji wa waraibu wa dawa za kulevya ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Alisema tatizo la dawa za kulevya linaendelea kuathiri mataifa mengi duniani hususan vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa, huku madhara yake yakijumuisha kuporomoka kwa afya, kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu, kudhoofika kwa uchumi wa familia na kupungua kwa tija katika uzalishaji.
Serikali kupitia DCEA imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, ikiwemo kuzuia biashara haramu ya dawa hizo, kutoa elimu kwa umma, kuimarisha huduma za tiba na uutengemao pamoja na kuanzisha ushirikiano wa kimkakati unaowawezesha waliopata nafuu kujenga upya maisha yao. Uzoefu unaonesha matibabu pekee hayatoshi ikiwa waraibu waliopata nafuu hawatapatiwa fursa za kujitegemea kupitia elimu, ujuzi wa kazi na kipato halali.
"Watu wengi wanaopata nafuu hukumbana na changamoto za ukosefu wa ajira, kipato na wakati mwingine kunyanyapaliwa na jamii. Changamoto hizi zinaweza kuwafanya kurejea tena kwenye matumizi ya dawa za kulevya endapo hawatapatiwa mbadala wa kujenga maisha yao. Ndiyo maana ushirikiano huu kati ya DCEA na VETA una umuhimu mkubwa katika kuwapa nafasi ya pili ya mafanikio," alisema Kamishna Jenerali Lyimo.
Kupitia makubaliano hayo, waraibu waliopata nafuu watapata nafasi ya kujiunga na vyuo vya VETA vilivyopo nchini kote kwa gharama nafuu ili kupata mafunzo katika fani mbalimbali zikiwemo useremala, umeme, ushonaji, ufundi magari, TEHAMA, upishi na taaluma nyingine zinazowawezesha kujiajiri au kuajiriwa. Matarajio ya Serikali ni kuona wahitimu wa programu hiyo wakipata vifaa vya msingi vya kuanzishia shughuli za uzalishaji kulingana na taaluma walizosomea, huku DCEA ikiendelea kushirikiana na taasisi za fedha zinazotoa mikopo midogo midogo ili kuwaunganisha na fursa za mitaji kwa ajili ya kuanzisha biashara na shughuli nyingine za kiuchumi.
"Tunataka waraibu waliopata nafuu wasibaki kuwa tegemezi kwa jamii. Tunawawezesha kupata ujuzi, ajira na kipato halali ili waweze kujitegemea, kurejesha heshima yao katika jamii na kuwa sehemu ya maendeleo ya Taifa," alisema.
Aliongeza kuwa mpango huo unatekeleza dhana ya kuwapa watu nafasi ya pili maishani kwa kuwawezesha waraibu waliopata nafuu kujenga upya maisha yao katika mazingira yenye matumaini na fursa.
Aidha, aliishukuru VETA kwa kukubali kushirikiana na DCEA katika kutekeleza mpango huo, huku akitoa wito kwa sekta binafsi, taasisi za kifedha, mashirika ya kiraia na wadau wengine kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha waraibu waliopata nafuu kupata ajira, mitaji na fursa nyingine za kiuchumi zitakazowawezesha kuishi maisha yenye tija.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Antony Kasore alisema, makubaliano hayo yanaonesha dhamira ya pamoja ya VETA na DCEA ya kutumia elimu ya ufundi stadi kama nyenzo ya kuwawezesha waraibu waliopata nafuu kujenga maisha mapya yenye matumaini na VETA ipo tayari pia kurasimisha ujuzi wa waraibu waliopata nafuu ambao tayari walijifunza fani mbalimbali kupitia mfumo usio rasmi kwa kuwapatia vyeti vitakavyotambua umahiri wao na kuongeza fursa zao katika soko la ajira.
Makubaliano hayo kati ya DCEA na VETA yanatarajiwa kuwa moja ya njia ya kupunguza uwezekano wa waraibu waliopata nafuu kurejea katika matumizi ya dawa za kulevya, kuongeza ushiriki wao katika shughuli za uzalishaji na kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa._1783943905.jpeg)
_1783943934.jpg)
_1783943952.jpeg)
_1783943965.jpeg)
