Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

Hotuba ya Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya James W. Kaji kwa Vyombo vya Habari. Tarehe 12 Machi 2020

17 March, 2020 Pakua

TAARIFA YA KAIMU KAMISHNA JENERALI WA MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA JAMES W. KAJI KWA VYOMBO VYA HABARI.

TAHEHE 12 MACHI 2020

Ndugu Wanahabari,

Tumewaiteni leo kuzungumza nanyi ili tuweze kuwapa mrejesho wa baadhi ya mafanikio ambayo nchi yetu imeyapata kutokana na juhudi za Mamlaka kwa kushirikiana navyombo vingine vya dola na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi. Tunawashukuru kwa mwitikio wenu chanya ambao ni ishara nzuri ya kuwa mnaunga mkono jitihada za Serikali katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini.

Tarehe 02 – 06 Machi mwaka 2020 nchi yetu ya Tanzania imeshiriki mkutano wa 63 wa Kamisheni ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Duniani (CND 63) uliofanyika Vienna, Austria. Nchi yetu ikiwa ni mwanachama tulipata nafasi ya kipekee kuelezea namna nchi yetu inavyopambana na tatizo la dawa za kulevya. Mkutano huu ambao una nchi wanachama 130 hukutana kila mwaka mwezi Machi jijini Vienna nchini Austria kujadili masuala mbalimbali ya udhibiti wa dawa za kulevya duniani na kutengeneza miongozo ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.

Katika mkutano huo Shirika la Umoja Wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) kupitia Kamisheni ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (CND), limeipongeza Tanzania kwa jitihada madhubuti katika kudhibiti na kupambana na tatizo la dawa za kulevya. Jitihada hizo madhubuti za nchi yetu katika kipindi cha miaka miatatu mfululizo kuanzia mwaka 2018 hadi 2020 na zimeleta matokeo chanya katika mapambano ya dawa za kulevya Duniani.

Pia ujumbe wa Tanzania ulioshiriki Mkutano huo ulipata nafasi ya kukutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja Wa Mataifa Linaloshughulikia Masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) Bi. Ghada Fathi Wally ambaye kipekee kabisa aliipongeza Tanzania kwa juhudi inazofanya katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya ambapo alisema, Tanzania ni moja kati ya nchi chache barani Afrika, zilizofanikiwa kupunguza upatikanaji na uhitaji wa dawa za kulevya pamoja na kupunguza madhara yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya. Vilevile mkuu huyo aliipongeza nchi yetu kwa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuweza kutekeleza mikakati minne ya kupambana na tatizo la dawa za kulevya kwa uwiano ulio sawa. Mikakati hiyo ni kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya, upatikanaji wa dawa za kulevya, kupunguza madhara yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya na ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya.

Ndugu Wanahabari,

Mafanikio haya yamekuja kutokana juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya marekebisho makubwa ya kisheria kwa kutunga Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Sheria Na.5 ya mwaka 2015 na mabadiliko yake ya mwaka 2017 kwa Tanzania Bara, na kwa upande wa Tanzania visiwani ambako mabadiliko ya sheria yamefanyika mwaka 2019.

Pamoja na kuwa na ukanda mrefu wa bahari na ukubwa wa mipaka, Tanzania imeimarisha udhibiti wa mipaka yake kwa kushirikiana vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa kufanya opereheni za mara kwa mara mipakani na majini ambazo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya nchini.

Kutokana na Mafanikio hayo, mwaka 2018 Shirika la Umoja Wa Mataifa Linaloshughulikia Masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) Liliipa Tanzania heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa kwa Kanda ya Afrika wa wakuu wa vyombo vinavyopambana na tatizo la dawa za kulevya (HONLEA 28) uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Mwl Nyerere jijini Dar es Salaam.

Aidha, taarifa ya UNODC ya mwaka 2019 inafafanua bayana kwamba Tanzania imefanikiwa kupunguza asiliamia 90 ya uingizaji wa dawa za kulevya hususani Heroin zilizokuwa zinaingia kupitia ukanda wa bahari. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa pamoja na vitengo vyake lina utaratibu wa kutoa taarifa za kila mwaka juu ya mwenendo wa tatizo la dawa za kulevya duniani.

Ndugu Wanahabari,

Pamoja na mafanikio haya makubwa, kwa masikitiko makubwa baadhi ya magazeti wanaichafua nchi yetu kwa kuandika habari zisizosahihi kuhusu udhibiti na mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Kimataifa nchi yetu imekuwa ni nchi ya mfano wa kuigwa, kwani hata nchi za Uganda, Msumbiji, Ghana, Nigeria na Norway zimeomba kujifunza kutoka kwetu mfumo wa utendaji kazi wetu pamoja na sheria yetu inavyofanya kazi.

Ndugu Wanahabari,

Gazeti la The East African toleo namba 1323 la tarehe 07 – 13 Machi 2020 na gazetila kimtandao la The Citizen la iliyotoka tarehe 08 Machi yameandika taarifa inayofanana ikisema Tanzania ni kitovu cha dawa za kulevya Afrika Mashariki. Taarifa hizo ni za upotoshaji na zinatakiwa kupuuzwa, Nchi yetu ni moja ya nchi zinazofanya vizuri katika kudhibiti na kupambana na tatizo la dawa za kulevya duniani kama nilivyoeleza hapo awali.

Napenda kuwakumbusha wanahabari ninyi ni nguzo muhimu sana katika jamii. Kazi yenu ya kutoa habari inaweza kuleta matokeo hasi ama chanya kwa jamii. Ni muhimu kuwa makini katika uandishi wa habari na ni vema kutumia vyanzo vya uhakika na kuzingatia maadili ya uandishi.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa mujibu wa sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya namba (5) kifungu cha 7(2) ina wajibu wa kutoa taarifa sahihi kwa jamii ya watanzania kuhusiana na masuala ya dawa za kulevya na vilevile vyombo vya habari kwa kifungu hiki vinawajibika kutoa habari sahihi kwa wananchi kinyume na hapo ni ukiukwaji wa Sheria.

Mamlaka iko wazi na tayari wakati wote kutoa ushirikiano kwenu hususani kuwapatia taarifa zilizo sahihi pia baadhi ya taarifa sahihi mnaweza kuzipata kupitia tovuti ya Mamlaka, na taarifa za dawa za kulevya kimataifa kupitia tovuti ya Shirika la Umoja Wa Mataifalinaloshughulikia masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC).

Ndugu Wanahabari,

Mamlaka inawashukuru kwa ushirikiano wenu ambao mmeuonesha kwa kuitikia wito kwa wingi na ninaomba tuendelee kushirikiana katika mapambano haya ambayo ni kwa manufaa ya Taifa letu kwa ujumla.

Asanteni kwa kunisikiliza