Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Waziri Balozi Dkt. Chana Atembelea Kituo cha MAT Mwananyamala

Imewekwa: 18 March, 2022
Waziri Balozi Dkt. Chana Atembelea Kituo cha MAT Mwananyamala

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewataka Waraibu wa dawa za kulevya kuendelea kutumia kliniki za MAT zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini kupata dawa ili waweze kurejea katika hali ya kawaida kwa ajili ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa.

Mheshimiwa Waziri Balozi Dkt. Chana ameyasema hayo siku ya Jumatano tarehe 15 Machi, 2022 alipofanya ziara katika kituo cha kutolea huduma ya Methadone (MAT clinic) kilichopo katika Hospitali ya Mkoa ya Rufaa Mwananyamala.

Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa, vijana wote wakiwemo waraibu wanaopona wananufaika kupitia fursa mbalimbali ikiwemo kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.

"Hata wale wenye changamoto, waraibu wanayo haki ya kujiunga katika vikundi wakapata fursa hii, na mikopo hii inatolewa pasipokuwa na riba ya aina yoyote. Hizi ni jitihada za Serikali yetu za kuwasaidia wanawake na vijana, hivyo fursa hizi zinatolewa katika vikundi, ni muhimu sana vijana wakajiunga katika vikundi, kwani umoja ni nguvu. Kikundi ndiyo dhamana ya kurudisha fedha hizo ili wengine wapate” amesema Dkt. Chana.

Pia ametoa wito kwa maofisa wa ustawi wa jamii kuwaunganisha waraibu na maafisa wanaoratibu utoaji wa mikopo kwa vijana na wanawake ili waweze kunufaika kupitia mikopo hiyo kwa ajili ya kwenda kuzalisha.

Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dkt. Zavery Benela amesema kuwa, Kliniki ya MAT Mwananyamala inahudumia Zaidi ya waraibu 1,350 kila siku ikiwemo kuwaelimisha vijana wote wanaopatiwa huduma ili baada ya kupona waweze kushiriki zaidi katika shughuli za uzalishaji mali kwa manufaa yao, jamii na Taifa.

Kamishina wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Dkt. Peter Mfisi wakati akijibu swali lilliloulizwa na mwandishi wa Habari amesema, hadi kufikia mwezi Desemba 2021, zaidi ya waraibu 10,600 walikuwa wamesajiliwa na kupata huduma kupitia vituo mbalimbali vya tiba saidizi kwa waraibu vilivopo nchini.

“Mpaka sasa kuna jumla ya vituo 15 ambavyo husimamiwa na Serikali na huhudumia waathirika wa dawa ya kulevya aina ya afyuni kama vile heroin na baadhi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya. Waathirika wanaotibiwa kwenye vituo hivi hutibiwa kwa kutumia dawa mfano Methadone. Waathirika wanatakiwa kuhudhuria matibabu kila siku mpaka watakapomaliza matibabu,"amesema Dkt.Mfisi.

Kuna faida nyingi za tiba ya methadone ikiwemo kundoa utegemezi wa dawa za kulevya aina ya heroin, kupunguza hatari ya mtegemezi kuwa katika hali ya kupata maambukizi ya HIV, homa ya ini na kifua kikuu.

Pia inaimarisha mwili na kumfanya mgonjwa kurudi katika hali yake ya kawaida na inaboresha mfumo wa mwili na kupunguza hatari za matumizi yasiyo sahihi ya dawa kwa kuzidisha kiwango ikiwemo kupunguza vifo vya ghafla.