Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Wawili kizimbani kwa kusafirisha bangi

Imewekwa: 10 July, 2020
Wawili kizimbani kwa kusafirisha bangi

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imewafikisha Mahakama ya hakimu mkazi Arusha watuhumiwa Seuri Kisambu (34) na Losieku Sirai Mollel (35) wakazi wa Mwandeti kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya bangi kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) na (3) (iii) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015 ikisomwa pamoja na aya ya 23 ya jedwari la kwanza la kifungu cha 57 (1) na 60 (2) ya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa Sura 200 kama ilivyorekebishwa na kifungu cha 16 (b) na 13 (b) cha sheria ya marekebisho ya mwaka 2016.

Washtakiwa walifikishwa mahakamani tarehe 08 Julai 2020 Mbele ya Hakimu Mkazi Gwantwa Mwinguka kwa ajili ya kusomewa mashtaka yao ya uhujumu uchumi yaliyosajiliwa mahakamani hapo kama mashauri namba 50 na 51 ya mwaka 2020.

Upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa tarehe 30 Juni 2020 katika kijiji cha Engilioni wilayani Arumeru mkoani Arusha, mshtakiwa Seuri Kisambu alikutwa akisafirisha kilo 649.5 za dawa ya kulevya aina ya bangi kinyume cha sheria na mshitakiwa Losieku Sirai Mollel alikutwa akisafirisha kilo 728.9 za dawa hizo.

Washitakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza mashauri hayo ya uhujumu uchumi. Mashauri hayo yataendelea kutajwa kwenye Mahakama hiyo kusubiri utaratibu wa kuyapeleka Mahakama Kuu divisheni ya makosa ya rushwa na Uhujumu uchumi.