Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

Watuhumiwa wa Dawa za Kulevya wahukumiwa

Imewekwa: 28 September, 2019
Watuhumiwa  wa Dawa za Kulevya wahukumiwa

Leo tarehe 27/09/2019 Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu Uchumi mkoani Mtwara imewahukumu kwenda jela watuhumiwa Mwinyi Kitwana Rajabu na Ally Hamdan Hamad miaka 20 kila mmoja kwa kosa la kusafirisha Dawa za Kulevya aina ya Heroin. Sambamba na adhabu hiyo Mahakama imetoa amri ya kutaifisha gari lililotumika kusafirisha dawa hizo.

Watuhumiwa hao Mwinyi Kitwana Rajabu, umri wa miaka 30, mkazi wa Magomeni Mapipa, Dar es salaam na Ally Hamdan Hamad, miaka 43, mkazi wa Mbezi Luis, Dar es salaam walikamatwa tarehe 07/11/2017 na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) eneo la mpaka wa Kalambo wilayani Mtwara vijijini Mkoani Mtwara wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin yenye uzito wa kilo 63.155 zilizokuwa zimefichwa kwenye gari aina ya TOYOTA Alphard yenye namba za usajili T499 DCL.

Watuhumiwa hao walifikishwa mbele ya Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu Uchumi mkoani Mtwara na kufunguliwa Shauri la Uhujumu Uchumi Na. 1 la mwaka 2018.

Shauri hili lilisikilizwa na Mheshimiwa Jaji Lilian Mashaka wa Makahama Kuu kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi huku upande wa mashtaka ukiongozwa na Saraji Iboru Wakili Mwandamizi wa Serikali na Kauli Makasi Wakili wa Serikali.

dawa za kulev

Wakati huo huo, jana tarehe 26/09/2019 Mahakama Kuu mkoani Songwe mbele ya Mheshmiwa Jaji Dkt. Adamu Mambi imemtia hatiani mtuhumiwa Waziri Shabani Mizogekwa makosa mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin yenye uzito gramu 1645.89 na mchanganyiko wa Heroin na Cocaine yenye uzito wa gramu 547.21.

Mtuhumiwa amehukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela na faini ya Tshs. 73,873,350/= kwa kosa la kwanza na miaka 20 na faini ya Tshs. 197,080,450/= kwa kosa la pili.

Hukumu hiyo imetolewa baada ya kuthibitishwa mahakamani kuwa mnamo tarehe 04/05/2012 majira ya saa 5 asubuhi huko katika nyumba ya kulala wageni ya NICE SHIREZ eneo la Tunduma wilayani Mbozi kwa wakati huo (sasa Momba) mkoani Mbeya (sasa Songwe)mtuhumiwa alikutwa chumbani kwake akiwa na dawa hizo.

Ushahidi huo uliwasilishwa mahakamani na mashahidi wa upande wa mashtaka ukiongozwa na Bw. Achiles Mulisa, Wakili wa Serikali Mwandamizi.

Aidha amri ya kuteketeza dawa hizo imetolewa kwa mahakama zote na zoezi la kuteketeza dawa hizo kwa upande wa Songwelitafanyikia Kiwanda cha Saruji jijini Mbeya huku utaratibu wa utekelezaji wa Dawa mkoani Mtwara unaandaliwa.