Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Watatu nguvuni kwa kusafirisha heroin Dar

Imewekwa: 01 February, 2021
Watatu nguvuni kwa kusafirisha heroin Dar

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inawashikilia wakazi watatu wa jiji la Dar es Salaam kwa kukutwa na dawa za kulevya aina ya Heroin yenye uzito wa gramu 400 pamoja na bangi.

Watuhumiwa hao ni Anadhati Rashid Mchongeza (20), Emmanuel Msakuzi (23) na Kulwa Pazi Shamas (49) almaarufu mama udodi, ambaye pia ni balozi wa nyumba 50 katika mtaa wa Juwaje, Kunduchi Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Mamlaka James Kaji amesema, watuhumiwa walikamatwa tarehe 22 Januari 2021 katika eneo la Kunduchi Pwani Kauzeni jijini Dar es salaam wakiwa na unga unaodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya Heroin kiasi cha gram 400 na majani makavu ya bangi puli moja kiasi ambacho kinaweza kutengeneza kete 30 za bangi.

Kamishna Kaji alisema maafisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya baada ya kufanya upekuzi walikamata dawa hizo zikiwa zimehifadhiwa ndani ya mfuko wa nailoni. ''Mamlaka inaendelea kuwashikilia watumumiwa na watafikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria kukamilika'' alisema Kaji.

Kadhalika kamishna Kaji amezungumzia mafanikio yaliyofanywa na Mamlaka katika kipindi cha mwezi Novemba mpaka Disemba mwaka jana ambapo alisema, '' DCEA tumefanikiwa kushinda kesi kubwa tatu zilizowahusisha mapapa wa biashara haramu ya dawa za kulevya Nchini''.

Ametaja majina ya mapapa hao kuwa pamoja na mfanyabiashara maarufu jijini Tanga Yanga Omari Yanga maarufu kama Raisi wa Tanga na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin kiasi cha gramu 1052.6

'' Mwingine ni Ayubu Mfaume Kiboko na Mkewe Pili Kiboko na kuwahukumu kifungo cha miaka 20 kila mmoja kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa gramu 251.25'' amebainisha Kaji.

Ameongeza ''Watuhumiwa wengine ni raia wawili wa Iran ambao walitiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin yenye uzito wa kilogramu 111.02 katika Bahari ya Hindi na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela pamoja na kutaifishwa kwa jahazi husika''.

Alisema, katika kipindi hicho pia, DCEA imefanya operesheni mbalimbali na kufanikiwa kumkamata Kibinda Mohamed Selemani akiwa na dawa za kulevya aina ya heroin kiasi cha gramu 135.12.Mtuhumiwa ameshafikishwa mahakamani.

Vilevile amesema mwaka 2020, Mamlaka imefanikiwa kufungua vituo vingine vitatu vya kutolea tiba ya methadone Tanga, Bagamoyo na hospitali ya Tumbi Pwani.

'' Mamlaka imeongeza wigo wa upatikanaji wa tiba ya uraibu wa dawa za kulevya kwa kuongeza vituo vingine vitatu vya kutolea tiba ya methadone “satellite clinics” jijini Dar es Salaam maeneo ya Segerea, Mbagala rangi tatu na Tegeta vinavyotarajia kuanza kutoa huduma hiyo mwezi ujao Februari, 2021. Hiyo inafanya Jiji la Dar es Salaam kuwa na jumla ya vituo sita (6) kati ya tisa (9) vinavyotoa tiba ya methadone nchini ili kupunguza msongamano uliokuwa katika vituo vitatu vya awali'' amesema Kamishna Jenerali Kaji.

Mamlaka inatarajia kuzindua kituo cha tiba ya methadone mkoani Arusha kitakachohudumia kanda ya Kaskazini. Mikoa mingine iliyokuwa na vituo vya tiba ya methadone ni Mbeya, Mwanza na Dodoma. Hadi sasa vituo hivi vimeweza kutoa huduma kwa waraibu 9,500 nchini.

Pia,huduma ya upataji nafuu inaendelea katika nyumba 25 “sober houses’ zilizopo maeneo mbalimbali nchini. Hadi kufikia mwezi Desemba 2020 kulikuwa na waraibu wapatao 3,663 walionufaika na huduma hiyo, kati yao 3,609 wakiwa wanaume na 74 wanawake.

Akizungumzia elimu na uelimishaji umma, Kaji amesema, Mamlaka inaendelea kutoa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya kwa njia mbalimbali ikiwemo matukio makubwa ya kitaifa na vyombo vya habari.

Katika kudhibiti na kuzuia uchepushwaji wa kemikali bashirifu zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya,Kaji amesema, ''Mamlaka kwa kushirikiana na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali tumetoa mafunzo kwa wadau mbalimbali zaidi ya 500 wakiwemo madereva wa malori, wasimamizi wa shughuli zinazohusu kemikali, wajasiriamali wanaotumia kemikali pamoja na maafisa biashara, na maafisa wa serikali wanaohusika kudhibiti wa kemikali hizo''.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inaendelea kuwakumbusha watanzania wote kutambua tatizo la dawa za kulevya kuwa ni mtambuka hivyo wadau mbalimbali pamoja na jamii kwa ujumla wanapaswa kutoa ushirikiano. ''Naomba kuchukua nafasi hii kuwaomba Umma kwa ujumla wake kushiriki kwa dhati kabisa katika kukabiliana na tatizo la matumizi na biashara ya dawa za kulevya nchini, hasa kuwafichua wanaojihusisha na biashara hii haramu'' amesema Kaji.