Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Mamlaka yawanoa waandishi wa habari za mtandao

Imewekwa: 11 November, 2021
Mamlaka yawanoa waandishi wa habari za mtandao

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imefanya kikao kazi cha siku tatu na waandishi wa habari za kimtandao kutoka katika vyombo vya habari thelathini (30), mkoani Morogoro. Lengo la kikao kazi hicho ni kuwapa elimu wanahabari kutumia mitandao ya kijamii kutoa taarifa sahihi juu ya tatizo la dawa za kulevya ili waweze kuwahamasisha vijana walio katika rika balehe walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya na UKIMWI kujiunga na vituo vya matibabu.

Wakati akiwasilisha mada juu ya Mamlaka na shughuli inayozifanya, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Mamlaka Bi. Florence Khambi amewataka wanahabari kutumia kalamu zao vizuri kuelimisha na kuhabarisha jamii kuhusu athari za matumizi na biashara ya dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa pale wanapombaini mtu anaetekeleza uharifu wa biashara ya dawa za kulevya..

"Mamlaka tunafanya kazi kutokana na jamii. Kwa niaba ya Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Gerald Kusaya niwahakikishie kuwa, mtu au watu ambao wataleta taarifa zao katika mamlaka zinazohusiana na uhalifu wa dawa za kulevya, tutazipokea kwa uaminifu wa hali ya juu na kuzifanyia kazi kwa usiri mkubwa” amesema Florence.

Aidha Bi. Khambi amesema kuwa, dira ya Mamlaka ni kujenga jamii ya Tanzania isiyotumia dawa za kulevya wala kushiriki katika biashara hiyo na hivyo kuchangia lengo kuu la kuwa na maisha bora nchini kama ilivyochagizwa kwenye malengo ya maendeleo ya 2025.

Kamishina Msaidizi Kinga na Huduma za Jamii wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) Moza Makumbuli wakati akiwasilisha mada kuhusu dawa za kulevya, madhara yake na matibabu kwa waathirika, alitoa wito kwa jamii kutokuwanyanyapaa waathirika wa dawa za kulevya, badala yake ijenge ukaribu nao na kuendelea kuwapa elimu juu ya madhara ya matumizi ya dawa hizo ili waweze kuondokana na hali hiyo.

Naye Kamishina wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Dkt. Peter Mfisi amesema utafiti umeonesha kuwa kati ya wanawake 100 wanaotumia dawa za kulenya nchini 61 kati yao wameambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU) kutokana na kuchangia sindano za kujidunga.

Pamoja na mada zilizotolewa, kikao kazi hicho kilitoa fursa kwa waandishi kuwatembelea waathirika wa dawa za kulevya ambao wapo chini ya uangalizi wa nyumba ya upataji nafuu (sober house) ya Free at Last iliyopo mjini Morogoro ili kujifunza namna waraibu wanavyoishi na kupata matibabu kwenye nyumba hizo.

Mmoja wa waraibu Abel Leonard ambaye anaendelea na uangalizi kutoka mkoani Mbeya amesema kuwa, hawafurahi kuwa katika hali hiyo, kwani hata yeye alijikuta ameangukia katika janga hilo baada ya kupoteza wazazi wote na kukosa marafiki wema wa kumuongoza.

Amesema, anajutia kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, kwani yamemvurugia mfumo wa maisha yake na anaamini akipona ataenda kuwa balozi mwema huko mtaani, kwa kuwa matumizi ya dawa hizo hayana faida badala yake amepoteza muda na kila kitu.

Naye msimamizi wa nyumba ya Free At Last, Michael Cassian amesema, jamii ikifanikiwa kuushinda unyanyasaji na unyanyapaa kwa waathirika wa dawa za kulevya huo utakuwa ni uponyaji tosha kwao. ukosefu wa elimu sahihi kwa jamii kuhusu watu waliothiriwa na dawa za kulevya umesababisha kukithiri kwa matukio ya udhalilishaji kwa waathiriwa ikiwemo kuigizwa na kuitwa majina yasiyofaa kama vile mateja na mengine mengi jambo ambalo halipaswi kuungwa mkono.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamabana na Dawa za kulevya inatambua mchango wa waandishi wa habari katika kuiangazia jamii juu ya masuala mbalimbali. Hivyo inaamini elimu “iliyopandwa” kwa vijana hawa wanaoviwakilisha vyombo vya habari 30 Thelathini Nchini inaweza kuliangazia suala zima la dawa za kulevya kwa namna iliyo sahihi hivyo kuleta mabadiriko chanya katika udhibiti wa ya tatizo la dawa za kulevya Nchini.