Vyombo vya Ulinzi na Usalama Mikoa ya Mbeya na Songwe Vyahamasishwa Kushiriki Katika Mapambano Dhidi ya Dawa Za Kulevya
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya – DCEA imefanya kikao kazi na Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, watoa huduma za afya, asasi za kiraia, na waraibu waliopata nafuu katika mikoa ya Mbeya na Songwe kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Akizungumza katika kikao kazi hicho, Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo amesema, ushirikiano kati ya Mamlaka na vyombo vya ulinzi pamoja na jamii kwa ujumla ni nguzo muhimu katika kuleta matokeo chanya katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwakuwa suala la dawa za kulevya ni mtambuka na linahitaji jitihada jumuishi.
Amesema, “wafanyabiashara wa dawa za kulevya wanaokamatwa sio wapya ni wafanyabiashara wa siku nyingi ambao wamekamatwa kutokana na ongezeko la operesheni, umakini na uzalendo wa Mamlaka pamoja na ushirikiano kati ya Mamlaka na vyombo vya dola. Hivyo, nawapongeza jeshi la polisi, jeshi la wananchi pamoja na vyombo vyote tunavyoshirikiana navyo kwa kuyafanikisha haya”.
Pamoja na hayo ameongeza kuwa Mamlaka imewekeza katika utoaji elimu kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo kuwafikia wanafunzi katika shule mbalimbali kwa kutumia klabu za TAKUKURU zilizoko shuleni ambazo kwa sasa zinaitwa klabu za kupinga rushwa na dawa za kulevya.
Aidha, washiriki walipata fursa ya kujifunza kuhusu tatizo la dawa za kulevya kupitia mada mbalimbali zilizowasilishwa pamoja na kuelezwa namna wanavyoweza kushiriki katika mapambano hayo. Mada zilizowasilishwa ni pamoja na majukumu ya DCEA katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya pamoja na operesheni zilizofanyika nchini, madhara ya dawa za kulevya, kuhusu matibabu sahihi kwa waraibu wa dawa za kulevya na umuhimu wake.