Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Umoja wa Mataifa Waipongeza Tanzania kwa Kudhibiti Tatizo la Dawa za Kulevya

Imewekwa: 17 March, 2020
Umoja wa Mataifa Waipongeza Tanzania  kwa Kudhibiti Tatizo la Dawa za Kulevya

Shirika la Umoja Wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) kupitia Kamisheni ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (CND), limeitaja na kuipongeza Tanzania kwa jitihada madhubuti katika kudhibiti na kupambana na tatizo la dawa za kulevya ambazo zimeleta matokeo chanya katika mapambano ya dawa za kulevya duniani katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2018 hadi 2020.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana an Dawa za Kulevya James Kaji amesema mafanikio hayo ya Tanzania yalibainishwa Katika mkutano wa 63 wa Kamisheni ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya duniani (CND 63) uliofanyika jijini Vienna – Austria ambapo maeneo yaliyotajwa kufanikiwa ni pamoja na kupunguza upatikanaji na uhitaji wa dawa za kulevya, kupunguza madhara yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya, na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

“Tuna kila sababu kama nchi kujipongeza. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya marekebisho makubwa ya sheria kwa kutunga Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na.5 ya mwaka 2015 na mabadiliko yake ya mwaka 2017 kwa Tanzania Bara, na kwa upande wa Tanzania visiwani mabadiliko ya sheria yamefanyika mwaka 2019. Pia tumefanikiwa kudhibiti mipaka yote ya ukanda wa bahari kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama”, amesema Kaji.

Aidha kamishna Kaji ametumia fursa hiyo kuviomba vyombo vya habari kuwa makini katika uandishi wa habari na ni vema kutumia vyanzo vya uhakika na kuzingatia maadili ya uandishi kwani kinyume na hapo ni uvunjaji wa sheria kwani upotoshaji wowote unakwamisha mapambano dhidi ya dawa hizi haramu.

Ikumbukwe kuwa taarifa ya UNODC ya mwaka 2019 inafafanua kwamba Tanzania imefanikiwa kupunguza asiliamia 90 ya uingizaji wa dawa za kulevya hususani Heroin zilizokuwa zinaingia kupitia ukanda wa bahari. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa pamoja na vitengo vyake lina utaratibu wa kutoa taarifa za kila mwaka juu ya mwenendo wa tatizo la dawa za kulevya duniani.