Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Tani mbili za bangi zateketezwa katika operesheni mbili jijini Arusha

Imewekwa: 03 July, 2020
Tani mbili za bangi zateketezwa  katika operesheni mbili jijini Arusha

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi imekamata na kuteketeza jumla ya magunia 140 ambayo ni zaidi ya tani mbili za dawa za kulevya aina ya bangi katika operesheni mbili zilizofanyika kijiji cha Engalauni na Lengilong wilayani Arumeru, jijini Arusha.

Katika tukio la kwanza lililofanyika kijiji cha Engalauni tarehe 30 Juni 2020, Mamlaka ilifanikiwa kuwakamata watu wawili ambao ni Bw. Sauli Kisambo Mollel (34) ambaye alikutwa amehifadhi gunia 32 za bangi nyumbani kwake na Bw. Losieku S. Mollel (35) kabila Mmasai ambaye nae alikutwa na gunia 33 za bangi, wote wakiwa ni wakazi wa Mandeki jijini humo.

Katika tukio la pili lililotokea tarehe 02 Julai 2020 Mamlaka imefanikiwa kukamata magunia mengine 75 yaliyokuwa yamehifadhiwakatika boma kijiji cha Lengilong ambapo wahusika wa dawa hizo wamezitekeleza na kutokomea kusikojulikana.

Hata hivyo, jumla ya magunia yote 140 yameteketezwa na maofisa wa Mamlaka kwa mujibu wa sheria na watuhumiwa wawili wanaoshikiliwa watafikishwa mahakamani muda wowote baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

g

Akizungumzia tukio hilo mbele ya vyombo vya habari wilayani Arumeru, Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka, James Kaji amesema ukamataji huu umefanikiwa kutokana na ufuatiliaji uliofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya maeneo hayo ikiwa ni katika moja ya operesheni zake za udhibiti na upambanaji wa dawa za kulevya Nchini.Pia amewaomba watanzania kuachana na biashara na kilimo haramu cha bangi.

‘‘Napenda kuwakumbusha watanzania wote hususan vijana ambao ndio kundi kubwa linalodanganyika na kujihusisha na dawa za kulevya ikiwemo kilimo haramu cha bangi kuwa, kujihusisha kwa namna yoyote ile na dawa za kulevya ni kosa kisheria. Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya [Sura ya 95] inatoa adhabu kali hadi kifungo cha maisha kwa atakayebainika kujihusisha na biashara hiyo. Hivyo, Mamlaka inaendelea kuwasihi Watanzania kutojihusisha kabisa na biashara hii haramu wala matumizi ya dawa za kulevya kwani atakayeshiriki atachukuliwa hatua stahiki’’ amesema Kaji.

J

Aidha, amesema Mamlaka iko macho na inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha inadhibiti uharifu wa dawa za kulevya Nchini. Hivyo kuwasihi wananchi kuunga mkono jitihada za Serikali katika kudhibiti tatizo la dawa za kulevya kwa kutafuta shughuli halali kwa ajili ya kujiingizia kipato na kutojihusisha kabisa na biashara hii haramu ambayo sio tu kwamba inarudisha nyuma jitihada za Serikali ya awamu ya tano katika suala zima la maendeleo kwa kuua nguvu kazi ya Taifa, bali pia inaharibu ustawi wa jamii bora ya watanzania.

Kaimu Kamishna Jenerali wa DCEA James Kaji akizungumza katika tukio la uteketezaji wa bangi wilayani Arumeru jijini Arusha