Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Taarifa ya Ukamataji wa Dawa za Kulevya Mwezi Septemba, 2019.

Imewekwa: 26 September, 2019
Taarifa ya Ukamataji wa Dawa za Kulevya  Mwezi Septemba, 2019.

Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za Kulevya nchini (DCEA) imefanikiwa kukamata Dawa za Kulevya aina ya Heroin zaidi ya kilo moja na nusu katika mikoa ya Dar es salaam na Mwanza, na zaidi ya kilo 214 za vifurushi vya dawa za kulevya aina ya mirungi zilizokuwa zikisafirishwa kwa njia ya posta kutoka Arusha kwenda nchini Uingereza katika mwezi septemba mwaka huu.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam, kaimu kamishna jenerali wa DCEA Bw. James W. Kaji amesema ukamataji huu wa usafirishaji wa vifurushi vya dawa za kulevya aina ya mirungi kwa njia ya posta ni muendelezo wa ukamataji uliofanywa na Mamlakakwa kushirikiana na Shirika la Posta, Wizara ya Kilimo na Mifugo na Wizara ya Mali ya Asili na Utalii nchini ambapo zaidi ya kilo 300 za dawa za kulevya aina ya Mirungi ilikuwa ikiingizwa nchini kutokea Ethiopia na kusafirishwa kwenda nchi za Ulaya hasa Uingereza kwa njia ya Posta, kwa kutumia majina bandia ya mlonge, moringa tea, dawa, majani ya mboga, tea leaves na moringa leaves.

Uchunguzi wa kimaabara kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ulithibitisha, majani hayo yana kemikali aina ya cathinone ambayo inapatikana kwenye mmea wa mirungi (Cath edulis). Taarifa za awali zilibaini kuwepo kwa usafirishwaji wa kiasi kikubwa cha dawa za kulevya aina ya mirungi kutoka nchini kwenda nchi za Ulaya kwa njia ya Posta, zikiwa zimepewa majina bandia, ambapo ilibainika dawa hizo ziliingizwa nchini kutoka nchini Ethiopia kama majani ya mlonge na kufungwa upya kisha kusafirishwa tena kwenda nchi za Uingereza, Canada, Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya. Awali, vifurushi hivyo vilikuwa vikisafirishwa kupitia Posta ya Dar es salaam na sasa vimekamatwa vikisafirishwa kupitia Posta Jijini Arusha

.

Makamishna wa Mamlaka katika mkutano wa waandishi wa habari

Aidha, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi inamshikilia aliyekuwa Afisa Usalama wa Shirika la Posta TanzaniaGeorge Arsein Mwamgabe kuhusiana na usafirshaji wa dawa za kulevya kwa njia ya Posta ambaye awali alitoweka kufuatia mahojiano yaliyokuwa yakiendelea dhidi yake. Pamoja na watuhumiwa sita (6) wanaohusishwa na dawa za kulevya aina ya Heroin uchunguzi wake umekamilika na watafikishwa Mahakamani.

Mamlaka inatoa rai kwa wale wote wanaojihusishana na biashara ya dawa za kulevya kuacha kwani mkono wa Sheria utawafikia popote walipo. Pia Mamlaka inawaomba wote wenye taarifa kuhusu dawa za kulevya kuiwasilisha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.