Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Shamimu, mumewe jela maisha kwa dawa za kulevya

Imewekwa: 08 April, 2021
Shamimu, mumewe jela maisha kwa dawa za kulevya

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi, imewahukumu washtakiwa Shamimu Omary Mwasha (43), na mume wake Abdul Issa Nsembo (47) kutumikia kifungo cha maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin hydrocloride zenye uzito wa gramu 275.40.

Pia mahakama hiyo imetoa amri ya kutaifishwa kwa gari aina ya Land Rover Discovery 4 yenye namba za usajili T.817 BQN kwa kuwa lilitumika kutekeleza uhalifu huo; pamoja na kuteketezwa kwa dawa walizokamatwa nazo.

Hukumu ya kesi hiyo, imetolewa na Jaji Elinaza Luvanda baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili kati ya Jamhuri na Utetezi na kujiridhisha kwamba watuhumiwa wamekutwa na hatia katika makosa mawili ya usafirishaji dawa za kulevya.

Kabla ya kuwasomea hukumu hiyo jaji Luvanda aliwasomea maelezo ya shauri hilo na kutupitilia mbali hoja kadhaa zilizotolewa na upande wa utetezi ikiwa ni pamoja na hoja iliyoeleza kuwa upekuzi haukufanyika kwa mpangilio maalumu kwani maafisa wa DCEA walikuwa wakiingia na kutoka hivyo huwenda vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani vilikuwa vimepandikizwa. Hata hivyo washtakiwa walishindwa kuweka bayana ni nani walikuwa wakiingia na kutoka .

Pia shamim alikana kuona kielelezo kikikamatwa katika nyumba yao wakati wa upekuzi kwani yeye alishuka chini kubembeleza watoto ingawa alikiri kuwa vikopo vinne vilivyokamatwa ni vipodozi vyake alivyokuwa anaviweka bafuni ila si dawa za kulevya.

Hata hivyo ushahidi uliotolewa na shahidi namba moja kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali aliipangua hoja hii kwa kuweka bayana vielelezo vilivyowasilishwa kwa mkemia na kuthibitisha kuwa vikopo viwili kati ya vinne vilikuwa na dawa za kulevya aina ya heroin hydrochloride.

Hivyo Kwa hiyo suala lililobaki lilikuwa ni je mfuko mweupe uliofungwa kwa nailoni ulikutwa kwenye gari? Na kikopo kilikutwa bafuni? Maswali hayo yote yalijibiwa katika ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa Jamhuri na kuthibitishwa,” amesema Jaji Luvanda

Aidha Jaji Luvanda alitupilia mbali hoja ya kwamba kulikuwa na shaka katika uwasilishaji wa vielelezo ambapo ameeleza kuwa vielelezo vyote vilioneshwa mbele ya mahakama tofauti na madai ya utetezi kwamba ni bahasha pekee ndiyo ziliwasilishwa mahakamani hapo bila dawa za kulevya.

Kabla ya kutolewa hukumu, upande wa Jamhuri uliiomba Mahakama itoe adhabu stahiki kwa washtakiwa kwani dawa za kulevya zina madhara makubwa kwa jamii na husababisha utegemezi na kupungukiwa akili. Kiasi walichokamatwa nacho kama kingeingia mtaani vijana wangeathirika badala ya kuinua uchumi wa nchi.Hata hivyo wakili msomi wa serikali Bi. Matikila aliieleza Mahakama kuwa hakuna kumbukumbu ya makosa ya jinai kwa washtakiwa wote wawili.

Kadhalika, upande wa utetezi kupitia mawakili Juma Nassoro na Hajra Mungula walisema washtakiwa wote wawili hawajaridhika na hukumu hivyo wanakusudia kukata rufaa. Pia waliomba huruma ya mahakama kwa kuzingatia kuwa washtakiwa hao ni wanandoa na wazazi wa watoto watatu wanaowategemea na wanaohitaji malezi ya wazazi na kuiomba mahakama itoe hukumu kwa kuangalia huruma hiyo hasa ukizingatia kuwa washtakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza.

Akitoa hukumu Jaji Luvanda amesema, ni kweli mshtakiwa namba moja na namba mbili ni wakosaji wa kwanza na kama ilivyoelezwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, na kuendelea kuwa sheria imetoa adhabu kwa makosa haya.

“Hivyo hakuna namna yoyote ya kutoa adhahu ya chini. Katika kosa la kwanza wanahukumiwa kifungo cha maisha gerezani, pia katika kosa la pili wanahukumiwa hivyo hivyo kifungo cha maisha gerezani, hivyo adhabu mtatumikia kwa pamoja,” amesema

Aidha Jaji Luvanda amesema kielelezo namba moja ambayo ni dawa za Kulevya kiteketezwe, kielelezo namba tano ambalo ni gari aina ya Land rover Discovery 4 kunataifishwa kuwa mali ya Serikali kwani ni mali ya mshtakiwa wa kwanza.

Nsembo na mkewe walikamatwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya tarehe 1 Mei, 2019 katika eneo la Mbezi Beach ‘A’ Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es salaam, wakiwa na kiasi hicho cha dawa za kulevya na kufunguliwa shauri la uhujumu uchumi namba 4 ya mwaka 2020 kwa kukiuka Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya Mwaka 2015 kama ilivyorejewa Mwaka 2019.