Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Serikali Yaomba Viongozi wa Dini Kukemea Matumizi ya Dawa za Kulevya

Imewekwa: 13 October, 2022
Serikali Yaomba Viongozi wa Dini Kukemea Matumizi ya Dawa za Kulevya

Serikali imetoa rai kwa viongozi wa dini kuendelea kuhimiza jamii kuepuka uraibu wa matumizi ya dawa za kulevya na kujenga uelewa sahihi kuhusu madhara ya dawa za kulevya.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti katika kipindi cha robo ya kwanza ya Mwaka 2022/23 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya UKIMWI na Dawa za Kulevya Mjini Dodoma.

“Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya, itaendelea kushirikiana na Wizara nyingine katika kuona namna nzuri ya kuandaa maudhui ya mtandaoni ili kuelimisha vijana kuhusu athari ya dawa za kulevya kama ambavyo Tume ya Kudhibiti UKIMWI inavyofanya”.

Tupo kwenye utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo imetoa maelekezo mahususi kuhusu kushughulikia dawa za kulevya, Amesema Naibu Waziri.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya UKIMWI na Dawa za Kulevya Dkt. Alice Karungi ameipongeza serikali kwa kiwango cha fedha kilichopelekwa kwenye Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kinachoendana na kwa kiwango cha fedha kilichokadiriwa wakati wa bajeti.

“Zoezi la kuwasaidia vijana wetu waliopata nafuu ya uraibu wa dawa za kulevya kwa kupatiwa mafunzo ya kukuza ujuzi; kama sehemu ya jitihada za Mamlaka, katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, liwe endelevu”.

Naye Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Musabila Kusaya amesema Mamlaka imeweka msukumo mkubwa katika kukabiliana dawa zinazotoka nje ya nchi kama vile heroin, cocaine na methamphetamine.

“Bangi imekuwa ikitumika kwa wingi kwa sababu inapatikana kwa bei nafuu na zinalimwa katika maeneo ya kujificha sana”.

Tamaa ya kupata fedha imekuwa ikichochea wananchi kulima bangi kulinganisha na mazao mengine hata hivyo udhibiti unaendelea.

“Tunashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Kilimo waweze kushauri wananchi badala ya kulima bangi walime zao gani ambalo litawasaidia kupata fedha nyingi.”



Naye Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Dkt. Leonard Maboko ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya UKIMWI na Dawa za Kulevya kwamba fedha za Global Fund zitatoka robo ya pili ya mwaka wa fedha 2022/23.

“Mradi wa Umoja wa Mataifa wa Kuhusisha UKIMWI kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa katika bajeti 2022/23 iliyoidhinishwa ya shilingi 2,132,610,000.00, tayari kiasi cha shilingi 1,090,849,597.00 zimepokelewa. Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (ATF) katika bajeti 2022/23 iliyoidhinishwa ya shilingi 1,880,000,000.00 fedha za ndani, tayari kiasi cha shilingi 469,992,000.00 zimepokelewa mwishoni mwa mwezi Septemba 2022 hivyo zitatumika katika robo ya pili ya mwaka (Oktoba – Desemba, 2022)”.

Naye Mhe. Asia Halamga ameomba serikali kubadili baadhi ya Sheria zinazowazuia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya iweze kufanya kazi zake kikamilifu.