Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Serikali Kuhakikisha Waathirika wa Dawa za Kulevya Wanapata Tiba

Imewekwa: 05 December, 2019
Serikali Kuhakikisha Waathirika wa Dawa za Kulevya Wanapata Tiba

Kaimu kamishna jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. James Kaji; amesema katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya nchini, serikali imejipanga kikamilifu kutoa tiba kwa waathirika/waraibu wa dawa hizo.

Hayo ameyazungumza leo jijini Mwanza alipotembelea kliniki ya Methadone kwa waathirika wa dawa za kulevya katika hospitali ya Sekou Toure ikiwa ni utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka katika suala la kinga na tiba.

Katika ziara hiyo Kamishna amepata nafasi ya kuzungumza na waraibu wanaopata huduma kituoni hapo na amewasihi kuzingatia na kufuata masharti ya tiba ili waweze kupata nafuu. ” wakati huu mnapoendelea na matibabu ni vizuri mkijikita katika tiba na kutojihusisha na uhalifu au kuendelea kutumia dawa hizi haramu; serikali iko pamoja nanyi na inajitahidi kuhakikisha mnapata matibabu ili mrudi katika ujenzi wa Taifa kwani nchi inahitaji vijana watenda kazi hasa katika kuelekea uchumi wa viwanda” amesema kamishna Kaji.

g

Huduma ya Methadone hutolewa kwa waathirika wa dawa za kulevya aina ya Heroin, ambapo vituo vinavyotoa huduma hiyo husimamiwa na serikali na matibabu kwa waathirika hutolewa bure kila siku mpaka watakapopata nafuu. Pamoja na huduma hii waathirika hupatiwa elimu na tiba ya magonjwa mengine ya kuambukiza kama vile VVU, homa ya ini na kifua kikuu.

Mpaka sasa tiba ya methadone inatolewa katika vituo sita nchini ambavyo vinapatikana hospitali ya Muhimbili, Mwananyamala, Temeke, hospitali ya rufaa ya Mbeya, hospitali ya rufaa ya mwanza na Itega; huku vituo vingine vikitarajiwa kufunguliwaBagamoyo, Kibaha na Tanga.