Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Sekta Binafsi Kushirikishwa katika Kupambana na Kemikali Bashirifu na Dawa tiba Zenye Asili ya Kulevya

Imewekwa: 18 October, 2019
Sekta Binafsi Kushirikishwa katika Kupambana na Kemikali Bashirifu na Dawa tiba Zenye Asili ya Kulevya

Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine za Udhibiti zikiwemo Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bohari ya Dawa (MSD), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), pamoja na Baraza la Famasi nchini (PC) wameendesha warsha ya ushirikishaji sekta binafsi katika kudhibiti uchepushaji wa kemikali bashirifu.

Warsha hiyo ambayo imedumu kwa siku tatu kuanzia tarehe 15 hadi 17 Oktoba, 2019 imeratibiwa na Serikali ya Tanzania pamoja na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za kulevya (INCB) na kufanyika katika ukumbi wa Harbour View jijini Dar es Salaam.

Lengo la warsha ni kutathmini utekelezaji wa mradi wa ushirikishaji Sekta binafsi katika kudhibiti uchepushaji wa kemikali bashirifu ili zisitumike katika kutengeneza dawa za kulevya. Katika Warsha hiyo washiriki kutoka nchi mbalimbali wamejifunza namna Serikali ya Tanzania ilivyofanikiwa kushirikisha sekta binafsi katika udhibiti wa kemikali bashirifu. Nchi zinazoshiriki katika warsha hiyo ni pamoja na Nigeria, Madagaska, Ethiopia, Rwanda, Burundi, Mauritius, Malawi, Zambia, Eritrea. Vilevile, warsha hiyo imehudhuriwa na wakufunzi kutoka Umoja wa Mataifa kupitia INCB pamoja na nchi za Ufaransa na Afrika ya Kusini.

washiriki wa warsha katika kikao

Akizungumza Katika ufunguzi wa warsha hiyo kamishna wa divisheni ya Ukaguzi na Sayansi Jinai Bi. Bertha Mamuya amesema kutokana na ushirikiano huu, kutakuwa na mikataba na watu wataohusika kutoa taarifa juu mbalimbali kwa Serikali pia ushiriano huu utatoa mwanya wa majadiliano linapotokea tatizo na kuangalia namna ya kulitatua.

''Kulikuwa na vikwazo vingi kwasababu serikali ilikuwa inawaona waingizaji na wasambazaji wa dawa kama sehemu ya tatizo lakini kumbe sivyo. kwahiyo kitendo cha serikali kutambua umuhimu wetu kama sehemu ya timu tukiungana tutafanya mambo yaende vizuri na kwa haraka'' .amesema mdau mmoja wa sekta binafsi aliyehudhuria warsha hiyo.

Kuanzia mwezi Januari 2019 hadi sasa, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imefanikiwa kutoa mafunzo kwa wadau zaidi ya 600 ambapo kati ya hao 342 wanajihusisha na Dawa tiba zenye asili ya Kulevya na 320 wanajihusisha na kemikali bashirifu.