Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Raia wa kigeni na mkewe wahukumiwa miaka 30 jela kwa bangi

Imewekwa: 12 April, 2021
Raia wa kigeni na mkewe  wahukumiwa miaka 30 jela kwa bangi

Watu wawili ambao ni Damian Jankowski Kryzstof raia wa Poland na mkewe Bi. Eliwaza Raphel Pyuza raia wa Tanzania wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa makosa matatu, kustawisha mimea 729 ya bangi, kusafirisha kilogramu 17.2 na kutumia aina hiyo ya dawa za kulevya.

Washtakiwa hao wametiwa hatiani kwa Sheria ya Kudhibiti na Kuambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya Mwaka 2015 kama ilivyorejewa 2019.

Mawakili wa Serikali Ignas Mwinuka, Verdiana Mlenza na Lilian Kowero waliieleza mahakama kuwa washtakiwa hao walikutwa wakifanya shughuli hizo za kulima, kutumia na kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha sheria.

Akitoa hukumu ya shauri hilo kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Mhe. Hakimu Bernazitha Maziku alisema kuwa, Mahakama hiyo imejiridhisha na ushahidi toka kwa Jamhuri ambao haukuwa na shaka na kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa hao.

Shauri hilo pia lililowahusisha washtakiwa Eliwaza R. Pyuza, Hanif Hassanal Kanani raia wa Tanzania mwenye asili ya kihindi na Boniface George raia wa Tanzania, ambao walitiwa hatiani kwa kosa la matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi na kupewa adhabu ya kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Tsh. 4,000,000 kila mmoja.

Pamoja na hukumu hiyo, Mahakama imetoa amri ya kutaifisha shamba ekari moja nusu lililopo njia panda ya Himo ambalo lilitumika kulima bangi, pesa taslimu shilingi 26,765,000/= alizokamatwa nazo Bw. Damian Jankowski, Simtank mbili za maji lita 2000 , na pikipiki aina ya KTM Adventure yenye namba za usajili MC 972 AAD.

Damian na wenzake walikamatwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) tarehe 08 mwezi Februari 2020 eneo la njia panda ya Himo wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na kufunguliwa kesi ya Jinai Namba 79 ya mwaka 2020. Washtakiwa walikamatwa wakiwa na bangi iliyo shambani, bangi iliyo katika hatua za kusindikwa na bangi iliyoongezewa thamani na kusindikwa mfano wa jam, ambayo huiuza kwa watalii Zanzibar, Nairobi, Dar es Salaam na nyingine huisafirisha kwenda Ulaya.