Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Raia wa kigeni akamatwa akilima bangi Kilimanjaro

Imewekwa: 14 February, 2020
Raia wa kigeni akamatwa akilima  bangi Kilimanjaro

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inamshikilia Damian Jankowski (40) raia wa Poland kwa kulima na kufanya biashara ya bangi kinyume cha Sheria.

Mtuhumiwa alikamatwa siku ya Jumamosi tarehe 8 mwezi Februari baada ya kuthibitika kuwa anafanya kilimo hicho eneo la njiapanda ya Himo mkoani Kilimanjaro huku shamba lake likiwa limezungushiwa ukuta mrefu. Mtuhumiwa amekamatwa akiwa na bangi iliyo shambani, bangi iliyo katika hatua za kusindikwa na bangi iliyoongezewa thamani na kusindikwa mfano wa jam, ambayo huiuza kwa watalii Zanzibar, Nairobi, Dar es Salaam na nyingine huisafirisha kwenda Ulaya.

Akizungumzia maisha ya mtuhumiwa alipokuwa nchini, Kamishna wa operesheni wa Mamlaka Luteni Kanali Fredrick Milanzi amesema, “Mtuhumiwa aliingia nchini mwaka 2016 akitokea Poland kama mtalii akiwa na VISA ya siku tisini (90) tu ila ameendelea kukaa nchini kwa kipindi chote mpaka alipokamatwa kwa utaratibu wa kurenew VISA yake kila inapokwisha.”Akiwa nchini Bwana Damian amekuwa akiishi na mwanamke Mtanzania ambaye wamefanikiwa kupata mtoto mmoja.

J

Taarifa zinasema kwamba mwaka jana mtuhumiwa alishirikiana na mke wake kunununua shamba maeneo ya Himo njia panda na kuliandikisha jina la mtoto. Kisha kulizungushia ukuta mrefu na geti linalofungwa muda wote jambo lililosababisha majirani kutojua kinachoendelea ndani ya ukuta huo.

Kaimu kamishna jenerali wa Mamlaka Ndg. James Kaji amethibitisha tukio hilo kwa kusema “tulipata taarifa kutoka kwa wananchi wema kwamba kuna mwekezaji mmoja raia wa Poland ambaye amekuwa akiendesha kilimo cha bangi. Alikuja kwa cover ya kufungua kituo cha watoto yatima pia baadae angejenga hoteli ya kitalii. Lakini baada ya kupata taarifa maofisa wa mamlaka walifanikiwa kukamata eneo hili pamoja na mtuhumiwa aliyekuwa nyumbani kwake, mkewe, rafiki yake na mtoto mdogo. Baada ya upekuzi kuna bangi ambayo ilikuwa tayari imechakatwa na kutengenezwa kama jam na nyingine kama asali ya Australia ambayo anauza sehemu mbalimbali na alikuwa akisubiri wateja wake kutoka nchi za Ulaya. ”Pia kamishna Kaji amesema mtuhumiwa alijaribu kutoa rushwa kwa maofisa ya Mamlaka ili kumuachia. Vijana wangu walipokuja kumkamata aliweza kutoa hadi shilingi milioni kumi ili mambo yaishe na akaahidi watakapokubaliana kila baada ya Mwezi atakuwa akitoa shilingi milioni 40,” Alisema Kaji.

Sampuli iliyopelekwa ofisi ya Mkemia mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi imethibitisha kuwa bidhaa zilizokamatwa ni bangi. Mtuhumiwa yuko mikononi mwa Mamlaka na atafikishwa Mahakamani muda wowote kwa hatua za Kisheria.

J

t