Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Operesheni Teketeza Mashamba ya bangi Arusha; Kamishna Jenerali Kusaya Azungumza

Imewekwa: 26 May, 2022
Operesheni Teketeza Mashamba ya  bangi Arusha; Kamishna Jenerali Kusaya Azungumza

Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Arusha, imeteketeza zaidi ya hekari 21 za mashamba ya bangi mkoani humo. Sambamba na uteketezaji huo, takribani kilo 720 za bangi zilikamatwa katika matukio mbalimbali, yaliyowahusisha wafanyabiashara wanne ambao wanashikiliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari tarehe 24 Mei, 2022 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Musabila Kusaya alieleza kuwa tarehe 20 Mei 2022 Mamlaka ilianza operesheni maalum katika wilaya ya Arumeru na Monduli mkoani Arusha iliyolenga kupambana na dawa za kulevya aina ya bangi na kuwasaka watu wote wanaomiliki mashamba ya bangi pamoja na wale wanaojihusisha kwa namna yoyote na biashara ya dawa za kulevya aina ya bangi.

‘’Tumefanikiwa kuwakamata wafanyabiashara ambao walikuwa wakisafirisha magunia ya bangi ambayo ni zaidi ya kilo 720. Katika operesheni hiyo jumla ya watuhumiwa wanne tumewakamata. Hawa ni wanaomiliki mashamba na tuliowakuta na magunia ya bangi wakiyasafirisha kutoka Monduli na Arumeru kuja jijini Arusha” amesema Kamishna Jenerali Kusaya.

Aidha, amesema operesheni hizi zitakuwa endelevu katika maeneo yote Nchini kuhakikisha aina zote za dawa za kulevya zinadhibitiwa. Ameendelea kusema kuwa, kwa hali ilivyo katika maeneo mbalimbali Nchini hususani mkoa wa Arusha bado anaimani yapo mashamba ya bangi pamoja na baadhi ya wananchi waliohifadhi magunia ya dawa hizo.

Vilevile, ametoa onyo kali kwa wananchi wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, kuachana na biashara hiyo na kutafuta biashara halali itakayompatia kipato, kwani Mamlaka haitawafumbia macho.

Pia, amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Mamlaka pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kutoa taarifa ‘’Jukumu lenu ninyi wananchi tuambieni nani,yupo wapi. anafanya nini na anajihusishaje na dawa za kulevya, sisi kama vyombo vya ulinzi na usalama tutakachokifanya taarifa yeyote ile tutakayoipokea tutaifanyia kazi kikamilifu ili wale wote wanaojihusisha na dawa za kulevya tuweze kuwatia mbaroni, wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na hatimaye kuhukumiwa kulingana na makosa yao” amesema Kusaya.

Pamoja na hayo, Kamishna Kusaya amewataka wasanii mbalimbali Nchini kutumia Sanaa zao kutoa ujumbe wenye elimu katika jamii na siyo kuhamasisha uvutaji wa bangi, kwani katika uimbaji wao au uandaaji wa muziki huwa kuna maigizo mbalimbali wanayafanya hivyo yaelekezwe katika kuelimisha jamii na siyo vinginevyo. ‘’Wasanii wetu wamekuwa wakifanya maigizo mbalimbali katika nyimbo zao, tunawaomba watumie vyema nafasi hiyo kwaajili ya elimu ya kuifunza jamii na isiwe vinginevyo, ikiwa kinyume tutawachukulia hatua za kisheria, Tunataka tuwe na Tanzania huru isiyokuwa na dawa za kulevya''. alisema Kusaya

Dawa za kulevya zinaweza kwisha pale ambapo kila Mtanzania atazichukia dawa hizo,huku akisema dawa hizo zina madhara kwa Taifa zima endapo kama biashara hiyo itakuwa inaendelea bila kutazama kwamba kuna athari gani nyuma yake’ amesisitiza Kamishna jenerali Kusaya.


s

Baadhi ya magunia yaliyokamatwa na dawa za kulevya aina ya bangi


s

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Kusaya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha


s

Moja ya shamba la bangi lililoteketezwa