Tani tisa za dawa za kulevya zakamatwa Desemba, 2025; basi la King Masai Tours lahusishwa
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 9,689.833 za dawa za kulevya, pikipiki 11 na magari matatu, likiwemo basi aina ya Scania la kampuni ya King Masai Tours, lililokuwa likitumika kusafirisha dawa za kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari Januari 8, 2026, Kamishina Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema katika operesheni iliyofanyika mtaa wa Wailes, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, DCEA ililikamata basi hilo likiwa na pakiti 20 za dawa za kulevya aina ya skanka zenye uzito wa kilogramu 20.03. Dawa hizo zilifichwa ndani ya balo la mitumba na kuhifadhiwa katika sehemu maalum iliyotengenezwa kwa makusudi ndani ya basi hilo. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa takribani nusu ya muundo wa basi hilo ulikuwa umefanyiwa marekebisho kwa lengo la kuficha dawa za kulevya.
Ameeleza kuwa basi hilo lenye namba za usajili za Jamhuri ya Msumbiji AAM 297 CA lilikuwa likifanya safari kati ya Nampula (Msumbiji) na Tanzania.
Katika tukio hilo, watuhumiwa wawili walikamatwa, ambao ni Amasha Iddi Mrisho (40), mkazi wa Buza, Dar es Salaam, pamoja na Seleman Juma Ally (32), raia wa Msumbiji. Aidha, mmiliki wa basi hilo, Mtanzania anayetambulika kwa jina la Martin Simon Kiando, anaendelea kufanyiwa mahojiano na vyombo vya usalama.
Kamishina Jenerali wa DCEA amesisitiza kuwa Mamlaka itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watu binafsi au makundi yanayotumia vyombo vya usafiri kufanikisha uhalifu wa dawa za kulevya, na ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya moto kuacha mara moja kufanya marekebisho ya vyombo hivyo kwa lengo la kukwepa sheria.
Kwa upande wake, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeeleza kuwa basi hilo halikusajiliwa nchini Tanzania baada ya kushindwa kukidhi vigezo vya usajili, na kusisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na DCEA na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika ukaguzi wa vyombo vya usafiri, hususan vinavyofanya safari za kuvuka mipaka.
Katika operesheni nyingine iliyofanyika eneo la Kinyerezi, mtaa wa Majoka, wilayani Ilala, DCEA iliwakamata watuhumiwa Erick Ernest Ndagwa (32), Paul Blass Henry (34) na Tido Emmanuel Mkude (35) wakiwa na bangi kilogramu 193.66, zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Mkoa wa Morogoro kuelekea Dar es Salaam.
Aidha, kufuatia ukaguzi wa kina uliofanyika katika kampuni za usafirishaji wa mizigo jijini Dar es Salaam, DCEA ilikamata pakiti 20 za dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilogramu 9.54, zilizokuwa zimefungwa na kuwasilishwa kama majani ya mwarobaini yaliyokaushwa. Dawa hizo zilikuwa zikisafirishwa kutoka Jamhuri ya Kenya kuelekea Australia.
Vilevile, kupitia operesheni mbalimbali zilizotekelezwa katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Morogoro, Tanga, Lindi, Kilimanjaro, Njombe, Kigoma na Arusha, DCEA imefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya heroin gramu 37.34, skanka kilogramu 1.015, bangi kilogramu 7,969.98 na mirungi kilogramu 1,363.701, pamoja na kuteketeza ekari 14 za mashamba ya bangi.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inaendelea kuwasisitiza wananchi kushiriki katika kutoa taarifa kuhusu viashiria vya biashara, usambazaji na usafirishaji wa dawa za kulevya, pamoja na kuwa makini kutojihusisha na usafirishaji wa mizigo wasiyoifahamu.
DCEA itaendelea kutekeleza operesheni nchi nzima kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, na kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika wote watakaobainika kujihusisha na uhalifu wa dawa za kulevya.


_1768546171.jpeg)
_1768546269.jpeg)