Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Naibu Waziri Ummy awapongeza watumishi wa DCEA

Imewekwa: 29 February, 2024
Naibu Waziri Ummy awapongeza watumishi wa DCEA

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga amewapongeza watumishi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kazi nzuri wanayofanya katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini.

Mhe. Nderiananga ametoa pongezi hizo wakati alipotembelea ofisi za Mamlaka makao makuu jijini Dar es Salaam leo tarehe 29 Februari 2024, akiambatana na  naibu katibu mkuu ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ndg. Anderson Mutatembwa  pamoja na Lina Kitosi, mkurugenzi msaidizi Idara ya Bunge na Siasa, Ofisi ya Waziri Mkuu.

Amesema amefurahishwa na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa kipindi kifupi chini ya uongozi wa Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.

"Ninawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya. Mmepiga hatua kubwa katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini. Hii ni kazi nzuri inayostahili pongezi," amesema Mhe. Nderiananga.

Ameongeza kuwa, Serikali inatambua umuhimu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya katika kuhakikisha jamii na taifa kwa ujumla vinakuwa salama na kuondokana na athari za dawa za kulevya ndiyo maana imeamua kuiimarisha Mamlaka kwa kuongeza bajeti yake.

Kwa mwaka 2022/2023 bajeti ya Mamlaka ilikuwa shilingi 9,847,415,000.00 na kwa mwaka 2023/2024 bajeti ya mamlaka iliongezeka na kufika Shs. 12,339,786,00.00," amesema.

Aidha, Mhe. Nderiananga amewataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na kuzingatia taratibu, Sheria na Kanuni katika utekelezaji wa majukumu yao ili kufikia malengo ya Mamlaka na Taifa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025, Mhe. Nderiananga amesema Mamlaka imefanya vizuri katika kutekeleza maagizo yaliyotolewa katika Ilani hiyo, na kusisitiza kuwekwa na kuboreshwa kwa mikakati ya kuelimisha jamii juu ya madhara ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Vilevile, Mhe. Nderiananga ametoa wito kwa jamii, wazazi na walezi kuhakikisha wanawalea watoto katika misingi inayofaa ili kuepuka watoto kutumbukia katika janga la matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Mamlaka Aretas Lyimo amemshukuru Mhe. Waziri kwa kutembelea Mamlaka na kuahidi kuwa, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya itaendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa ufanisi zaidi katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini.