Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Miaka 30 jela kwa kusafirisha Heroin gramu 43.95

Imewekwa: 05 February, 2021
Miaka 30 jela kwa kusafirisha Heroin gramu 43.95

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa hukumu ya kifungo cha miaka thelathini (30) jela kwa mshtakiwa Linna Romani Maro (47) kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin hydrochloride zenye uzito wa gramu 43.95.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 2 Februari 2021 na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Agustina Mbando mara baada ya ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka kuthibitisha pasipo shaka yoyote kuwa, mshtakiwa alikamatwa na dawa za kulevya. Pamoja na adhabu hiyo, Mahakama imeamuru kutaifishwa kwa simu nne alizokuwa nazo mshtakiwa.

Linna alikamatwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya tarehe26 Januari 2018 eneo la Tabata Bima lililopo katika halmashauri ya wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam akiwa na kiasi hicho cha dawa za kulevya na kufunguliwa kesi ya Jinai Namba 295 ya mwaka 2018. Hivyo kutiwa hatiani kwa kufanya biashara ya dawa za kulevya kinyume na Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015 kama ilivyorejewa na Sheria Namba 15 ya mwaka 2017.