Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Mfanyabiashara Maarufu Dar Kizuizini Kwa Tuhuma za Kujihusisha na Biashara ya Dawa za Kulevya

Imewekwa: 03 January, 2020
Mfanyabiashara Maarufu Dar Kizuizini Kwa Tuhuma za Kujihusisha na Biashara ya Dawa za Kulevya

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) inamshikilia mfanyabiashara Abuu Saleh Kimboko mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam na Pascal Peter Lufunga mkazi wa Kibaha Pwani kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya.

Abuu Saleh Kimboko amekamatwa Desemba 29 mwaka 2019 akiwa maeneo ya Mbagala Zakiem/ Mpakani, jijini Dar es Salaam akiwa na dawa za kulevya aina ya heroin gramu 400 pamoja na bastola moja na risasi za moto 15 na vyote amekutwa navyo akiwa kwenye gari namba T568 DKC aina ya Toyota Spacio.

Akizungumza mbele ya wanahabari Januari mosi mwaka huu, kaimu kamishna jenerali wa Mamlaka James Wilbert Kaji amesema mfanyabiashara Kimboko ni miongoni mwa watuhumiwa waliokuwa wakitafutwa nchi mbalimbali kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

"Huyu jamaaa alikuwa anatafutwa kwa muda mrefu sana, na si Tanzania tu bali hata nchi nyingine nako walikuwa wanamtafuta kutokana na kujihusisha na bishara hii haramu.Kwa namna ambavyo Mamlaka na vyombo vya ulinzi na usalama kujipanga vema katika mapambano ya dawa za kulevya, tumemnasa na sasa tunamshikilia. Kwa wanamfahamu huyu Abuu kwa jina lingine la mjini tunaita Kipusa ndio anamiliki magari yaliyoandikwa Mashaallah,"amesema Kamishna Kaji.

Pamoja na mtuhumiwa huyo, Mamlaka inamshikilia pia Pascal Lufunga kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya . mtuhumiwa amekamatwa akiwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 133.33 eneo la Bwilingu Kibaha.

Watuhumiwa wote wako ndani na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.

Kamishna Kaji ametoa onyo kwa wanaojihusisha na biashara hiyo kuacha mara moja kwani lazima watakamatwa na huo ndio utakuwa mwisho wao. Pia ameiomba jamii kuendelea kuwafichua wanaofanya biashara hii haramu ili kuokoa kizazi cha watanzania hasa vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.

Kwa mwaka 2019, Mamlaka imefanikiwa kufanya operesheni mbalimbali na kufanikiwa kukamata dawa za kulevya kiasi cha kilo 325.69 za bangi zikiwahusisha watuhumiwa wawili, kilo 892.24 za mirungi zikiwahusisha watuhumiwa tisa na kilo 34 .47 za heroin zikiwahusisha watuhumiwa watano huku kesi 35 za dawa za kulevya zimemalizika katika Mahakama Kuu na dawa zilizohusika na kesi hizo zilishateketezwa.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya kwa kushirikiana na ofisi ya Mashitaka ya Taifa imefanikiwa kushinda mashauri kadhaa makubwa ya dawa za kulevya na miongoni mwa mashauri hayo ni lile lilihusu kilo 63 za heroin ambalo iliendeshwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara ambapo watuhumiwa Mwinyi Kitwana Rajabu na Ally Hamduni Hamad walihukumiwa kifungo Cha miaka 20 jela na kutaifishwa gari iliyohusika kusafirisha dawa za kulevya.