Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

RC Mtanda Afungua Maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya

Imewekwa: 28 June, 2024
RC Mtanda Afungua Maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Saidi Mtanda leo tarehe 28 Juni, 2024 amewakaribisha watanzania hususani wakazi wa mkoa wa Mwanza na maeneo jirani kujitokeza katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya ambayo yanafanyika kitaifa mkoani Mwanza katika uwanja vya Nyamagana ambapo mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho hayo akitarajiwa kuwa Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Akizungumza wakati akifungua Maadhimisho hayo yanayoongozwa na Kauli mbiu “Wekeza kwenye kinga na tiba dhidi ya dawa za kulevya” Mhe. Mtanda amesema tatizo la dawa za kulevya limezidi kuongezeka hivyo pia kuchangia maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na kwamba ni wajibu wa kila   mmoja kuhakikisha anapiga vita uuzaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya. Mhe. Mtanda amesema Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kupambana na dawa za kulevya ikishirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na wadau waliowekeza nguvu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

"Hongereni sana Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kazi nzuri mnayofanya katika kudhibiti uuzaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya, mmeonesha dhahiri kuwa mmejipanga vizuri kutekeleza majukumu yenu. Ni wajibu wa wadau mbalimbali kushirikiana na DCEA kupiga vita dawa za kulevya",amesema Mhe. Mtanda.

Aidha, akitaja sababu za kuadhimisha Maadhimisho haya yanayofanyika kila mwaka amesema,

‘‘Kwanza ni kutoa fursa kwa wananchi wa mkoa wa Mwanza na watanzania kupata elimu kuhusiana na athari za dawa za kulevya ambazo ni nyingi sana. Mnafahamu mtu yoyote anapotumia dawa za kulevya anaathirika kisaikolojia, kiakili, kimwili na hawezi kushiriki katika maendeleo yake binafsi wala taifa kwa ujumla. Pia, fedha nyingi zinatumika kuwatibu waathirika wa dawa za kulevya hivyo kuathiri pia Uchumi wa taifa”.

Pia amesema, Maadhimisho haya hufanyika kutambua jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya nchini.

“Ni lazima watanzania wajue serikali yao inafanya nini katika kupambana na tatizo hili ili kuhakikisha kwamba hakuendelei kuwa na dawa za kulevya nchini. Hivyo nawasihi watanzania hususani wakazi wa Mwanza kutumia fursa hiyo kuanzia leo tarehe 28 hadi 30 Juni, Kutembelea uwanja ya Nyamagana kwa ajili ya kupata elimu hiyo”.

Aidha, Mhe. Mtanda amesema pamoja na uzinduzi huo wa maadhimisho hayo kesho tarehe 29 Juni, kutakuwa na kongamano maalumu la kitaifa juu ya tatizo la dawa za kulevya ambalo litafanyika katika ukumbi wa Mkuu wa mkoa na kuhudhuriwa na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imetekeleza shughuli mbalimbali kuelekea Maadhimisho haya ikiwemo uelimishaji kupitia vyombo vya habari nchini, kusafisha mazingira na kushiriki katika kipindi cha malumbano ya hoja kinachorushwa na kituo cha ITV.

Mkuu wa Mkioa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda akizungumza na wananchi wa mkoa wa Mwanza katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya.

 Kikundi cha ngoma cha jijini Mwanza kikiburudisha wananchi katika ufuguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo akitoa salamu kwa wananchi katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya.

 

Mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda akipata Maelezo katka banda la Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wakati akikagua mabanda wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza MHE. Said Mtanda akisaini kitabu cha wageni katika banda a Mamlaka huku akisuhudiwa na kamishna jenerali wa DCEA Aretas Lyimo.